Marekani kuitumia Israel mamia ya mabomu aina ya MK-82
Serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani inapanga kutuma shehena za mabomu na silaha nyingine zenye thamani ya makumi ya mamilioni ya dola kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kumwaga damu za Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Ripoti ya jana Ijumaa ya gazeti la Wall Street Journal imesema kuwa, utawala wa Biden unatathmini suala la kuipa Israel silaha za zana mbali mbali za kijeshi yakiwemo mabomu 1,000 aina ya MK-82 yenye uzani wa pauni 500.
Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Vita wa Israel, Yoav Gallant alisema jana Ijumaa kuwa, utawala huo wa kibaguzi unapanga kuanzisha operesheni ya nchi kavu katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Hatua ya Marekani ya kuendelea kuisheheneza Israel kwa silaha wakati mwingine hata bila ridhaa ya Kongresi imekosolewa vikali na duru mbali mbali duniani, yakiwemo hata madola waitifaki wa Washington.
Wiki iliyopita, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alitoa wito kwa washirika wa utawala wa Israel kukomesha upelekaji silaha kwa utawala huo ghasibu iwapo wanataka kupunguza vifo vya raia vinavyosababishwa na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Ifahamike kuwa Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa zaidi wa Israel, huupatia utawala huo wa Kizayuni msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8 kila mwaka.
Aidha, tangu Oktoba 7,2023 Washington imeipatia Tel Aviv silaha zaidi ya tani 10,000 pale utawala huo haramu ulipoanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.