Feb 18, 2024 11:05 UTC
  • Biden aambiwa: Sitisha vita Gaza iwapo unataka kura za Waislamu

Meya wa jiji la Dearborn, kaunti ya Wayne katika jimbo la Michigan nchini Marekani amesema Rais Joe Biden wa hiyo hatapata kura za Waislamu katika uchaguzi ujao nchini humo, iwapo ataendelea kuunga mkono jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza.

Ripota wa IRNA mjini New York amemnukuu Abdullah Hammoud, Meya wa mji wa Dearborn ambao una jamii kubwa ya Waislamu na Waarabu akisema kuwa, "Hivi sasa, kitu sahihi cha kufanya ni kutoa mwito wa kusitishwa vita, kukata misaada ya kijeshi na uungaji mkono kwa Benjamin Netanyahu na kambi yake ya mrengo wa kulia, na vile vile kupeleka misaada ya kibinadamu (Gaza) kupitia UNRWA."

Hammoud ambaye amewahi kuwa Mwakilishi wa Michigan katika Bunge la Wawakilishi la Marekani, amemuasa Biden achukue hatua madhubuti za kuonyesha azma na irada njema ya kisiasa kwa jamii ya Waislamu, iwapo anataka uungaji mkono wao katika uchaguzi ujao. 

Tayari Waislamu wa Marekani wameanzisha kampeni ya kumsusia Biden kwenye uchaguzi huo wakisisitiza kuwa, mstari wao mwekundu ni kuendelea kusaidiwa na kuungwa mkono utawala haramu wa Israel katika vita vya Gaza. 

Abdullah Hammoud, Meya wa mji wa Dearborn

Rashida Tlaib, mwakilishi katika Bunge la Marekani mwenye asili ya Palestina, hivi karibuni aliweka video kwenye ukurusa wake wa mtandao wa kijamii wa X, akikosoa utendaji wa Biden wa kuunga mkono "kampeni ya mauaji ya halaiki ya Israeli huko Palestina" na kuandika: Usitegemee kura zetu katika uchaguzi wa mwaka huu (2024), na endapo hali hii itaendelea yumkini ikulu ya White House ikachukuliwa na chama hasimu cha Repulican.

Matokeo ya uchunguzi mpya uliofanywa na shirika la habari la ABC na Taasisi ya Utafiti ya Ipsos yanaonesha kuwa, asilimia 86 ya Wamarekani wanaamini kuwa Biden hana hadhi ya kuendelea kuweko kwenye Ikulu ya nchi hiyo. 

 

Tags