Feb 26, 2024 11:47 UTC
  • Ukraine yakanusha uvumi kwamba Iran imeiuzia Russia makombora ya balestiki

Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Jeshi la Ukraine amekadhibisha uvumi kwamba Iran imeiuzia Russia makombora ya balestiki kwa ajili ya kutumika katika vita vya Ukraine.

Mnamo tarehe 21 Februari, shirika la habari la Reuters lilidai kwamba, limezinukuu duru za kuaminika zikieleza kuwa Iran imeipatia Russia makombora 400 ya balestiki ya kushambulia kutoka ardhini hadi ardhini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha mara kadhaa madai ya nchi za Magharibi kwamba imeipatia Russia ndege zisizo na rubani au makombora kwa ajili ya kuyatumia katika vita vya Ukraine na kubainisha kwamba, ushirikiano wake wa kijeshi na Russia hauhusiani na vita vya Ukraine na unafanyika katika fremu ya uhusiano wa kiulinzi baina ya pande mbili.
Iran na Russia zina uhusiano wa kistratejia wa kiulinzi

Kairlo Budanov, Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Jeshi la Ukraine amekanusha madai ya nchi za Magharibi ya kusafirishwa makombora ya masafa marefu kutoka Iran kuelekea Russia kwa ajili ya kutumika katika vita vya Ukraine na akasema, hakuna kombora lolote la Iran ililopatiwa Russia; na habari zote zilizotangazwa kuhusiana na suala hilo si sahihi.

Afisa huyo mwandamizi wa Intelijensia wa Ukraine ameongeza kuwa, ni idadi ndogo tu ya makombora ya Korea Kaskazini iliyopokea Russia ndiyo yaliyotumika katika vita vya Ukraine, na madai kwamba "yametumika kwa wingi" hayana ukweli wowote.
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa naye pia alitangaza mnamo Februari 23 kwamba, japokuwa hakuna kizuizi chochote kisheria cha uuzaji wa makombora ya balietiki, lakini kimaadili, Iran inawajibika kujiepusha na kufanya miamala ya uuzaji silaha wakati wa vita kati ya Russia na Ukraine ili kuepusha kukolea zaidi moto wa vita hivyo; na hii inatokana msimamo wa Iran wa kuheshimu sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.../

 

Tags