Feb 29, 2024 07:12 UTC
  • Madeleine Dean
    Madeleine Dean

Mjumbe wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani amepinga mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Palestina na kumtaja Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu kuwa ni mhalifu na mwongo.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, Madeleine Dean, mwakilishi wa Kongresi ya Marekani ambaye hivi karibuni alisafiri katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) ameongeza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza ni makubwa zaidi kuliko inavyoakisiwa kwenye vyombo vya habari.

Mjumbe huyo wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema kuwa ukosefu wa uaminifu wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ukiukaji wa ahadi yake ya kutoshambulia raia na madai ya uongo kuhusu kutengwa maeneo salama huko Gaza, havikubaliki.

Gaza

Utawala wa Kizayuni wa Israel na viongozi wake watenda jinai wamekuwa wakilaaniwa na watetezi wa haki za binadamu kote duniani hususan baina ya Waislamu tangu utawala huo ulipoasisiwa, lakini sasa kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala huo ghasibu katika Ukanda wa Gaza, idadi ya wapinzani wa utawala huo pia imeongezeka miongoni mwa wasiokuwa Waislamu duniani.

Marekani ndiyo mfadhili na muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni, ambapo licha ya kutuma silaha na misaada ya kifedha kwa Israel, inatumia kura ya veto kwa ajili ya kupinga maazimio yote ya kimataifa yanayolaani uhalifu wa Israel na kutoa wito wa kusitishwa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 imefikia watu karibu elfu 30, na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu elfu 70,325.

Tags