Mar 22, 2024 06:59 UTC
  • Axios: Netanyahu atasusiwa na sehemu kubwa ya wawakilishi wa Congress

Tovuti ya habari ya Marekani ya Axios imesema kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huenda akasusiwa pakubwa na "wabunge wa Congress ikiwa atakubali mwaliko wa kuzungumza mbele ya Bunge la Marekani.

Tovuti hiyo imewanukuu wawakilishi wa chama cha Democratic, Chuy Garcia, Maxwell Frost, na Jamaal Bowman wakisisitiza kwamba hawatahudhuria hotuba ya Netanyahu katika Congress.

Frost ametetea msimamo wake kwa kusema kwamba, Netanyahu ni "mtu mbaya," wakati mwakilishi wa Kidemokrati, Annie Kuster, akisema kwamba watu wamekatishwa tamaa na jinsi vita vya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza vinavyoendeshwa.

Kwa upande wake, mbunge Jamaal Bowman amesema katika taarifa yake kwa Axios kwamba wapiga kura wake wana hasira kuhusu vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo tovuti ya habari ya Axios imemnukuu mwakilishi wa chama cha Democratic, Rashida Tlaib akisema kwamba: "Netanyahu hapaswi kuja kwenye Congress, bali anapaswa kupelekwa The Hague, akimaanisha Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Rashida Tlaib: Netanyahu apelekwe The Hague

Tovuti ya Punchball News iliripoti Jumatano iliyopita kwamba Kiongozi wa Wengi katika Seneti ya Marekani, Chuck Schumer, amekataa ombi la Netanyahu la kuzungumza mbele ya kambi ya Wademokrati katika Seneti.

Jumuiya za kutetea haki za binadamu zinatoa wito wa Waziri huyo Mkuu wa Isarel kupelekwa katika mahakama za kimataifa kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo haramu dhidi ya raia wa Palestina.

Hadi sasa karibu Wapalestina elfu 32 wameuawa na wengine zaidi ya elfu 72 kujeruhiwa katika mauaji ya kikatili yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza.  

Tags