Apr 29, 2024 02:35 UTC
  • Wasiwasi wa Russia kuhusu kusambaa zaidi ugaidi kutokea Afghanistan

Waziri wa Ulinzi wa Russia ametangaza kuwa tishio kuu kwa Asia ya Kati ni kutoka kwa makundi ya kigaidi yenye misimamo mikali yenye makao makuu nchini Afghanistan.

Sergei Shoigu amesisitiza katika kikao cha mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan kuwa, nchi za Asia ya Kati zinatishiwa na makundi ya kigaidi yaliyoko Afghanistan. 

Hii sio mara ya kwanza kwa maafisa wa kisiasa na kijeshi wa Russia kuelezea wasiwasi wao juu ya usafirishaji wa ugaidi kutoka Afghanistan hadi nchi nyingine za eneo la Asia ya Kati. Kwa mtazamo wa Russia, mchakato wa kuhamisha hali ya ukosefu wa usalama kutoka Afghanistan hadi maeneo mengine ya Asia ya Kati unajumuisha kesi mbalimbali kama vile biashara ya madawa ya kulevya, hasa heroini, silaha, magendo ya binadamu na matukio mengine ya ukatili. Rais wa Russia pia amekuwa akionya mara kwa mara kuhusu biashara ya madawa ya kulevya kuelekea nchini humo.

Tahmina Iqbal, mtaalamu wa masuala ya kieneo anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Ingawa vitisho vya kigaidi kutoka ndani ya Afghanistan havizilengi nchi za Asia ya Kati pekee, lakini matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Russia kuhusiana na suala hilo yanaonesha kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai bado ina wasiwasi wa usalama kuhusu ugaidi kutoka Afghanistan; na ili kukabiliana na janga hilo shirika hili inajaribu kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya wanachama wake."

Sergei Shoigu

Awali, Waziri wa Ulinzi wa Russia alisema kwamba mashirika ya kimataifa ya kigaidi yanaongeza ushawishi wao nchini Afghanistan, na nchi za Magharibi zinafanya kazi kikamilifu na makundi yenye silaha yaliyo nje ya nchi hiyo. Hii ina maana kuwa, Russia ina wasiwasi mkubwa kuhusu siasa za uingiliaji kati za nchi za Magharibi hususan Marekani katika masuala ya usalama wa eneo la Asia ya Kati kwa sababu kuna dhana katika eneo hilo kwamba, Marekani iliondoka Afghanistan kwa lengo la kuyaimarisha makundi ya kigaidi, ili makundi hayo yajipange upya katika nchi hiyo na kuhatarisha usalama wa eneo hilo hasa Asia ya Kati.

Kwa mtazamo wa Moscow, malengo ya nchi za Magharibi ya kuzidisha ushirikiano na makundi yenye silaha yanayopinga utawala wa Taliban nje ya Afghanistan pia yako wazi. Kwani nchi hizo zinajaribu kuunda kituo cha migogoro katika maeneo ya mpakani ya washirika wa Russia. Suala ambalo linachochea sana wasiwasi wa usalama katika eneo hilo. 

Ingawa Taliban wamekuwa wakidai mara kwa mara kwamba hakuna nchi inayokabiliwa na vitisho kutokea Afghanistan na kwamba kundi la kigaidi la ISIS limeangamizwa katika nchi hiyo, lakini wasiwasi uliotangazwa na maafisa wa ulinzi wa nchi wanachama wa Shanghai kuhusu tishio la ugaidi kutoka Afghanistan unaonyesha kuwa hawaamini matamshi hayo. Hasa, ikitiliwa maanani kwamba, Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, hapo awali alisema kuwa kundi la kigaidi la ISIS, linalenga kudhoofisha usalama wa nchi za Asia ya Kati kwa msaada wa vikosi vya majeshi ya kigeni.

Maria Zakharova

Zakharova alisisitiza kuwa ufadhili wa kundi la kigaidi la ISIS nchini Afghanistan unafanywa na idara za ujasusi za nchi za kigeni, na kwa mujibu wa tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, Marekani ndiyo inayoyafadhili makundi ya kigaidi ya ISIS na Al-Qaeda nchini Afghanistan.