Jumuiya za Kiislamu Marekani zapinga propaganda chafu katika vitabu vya shule
https://parstoday.ir/sw/news/world-i11173-jumuiya_za_kiislamu_marekani_zapinga_propaganda_chafu_katika_vitabu_vya_shule
Kundi linalojumuisha jumuiya 15 kubwa za Kiislamu nchini Marekani limelalamikia kitendo cha kuwekwa propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika vitabu vya shule za jimbo la California.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 13, 2016 15:19 UTC
  • Jumuiya za Kiislamu Marekani zapinga propaganda chafu katika vitabu vya shule

Kundi linalojumuisha jumuiya 15 kubwa za Kiislamu nchini Marekani limelalamikia kitendo cha kuwekwa propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika vitabu vya shule za jimbo la California.

Kundi hilo limeiandikia barua Taasisi ya Elimu ya jimbo la California likitangaza kuwa, kuwekwa propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika vitabu vya wanafunzi ambazo zinatengeneza muundo wa kifikra na kimwenendo wa wanafunzi hao kutakuwa na madhara kwa wanafunzi wenyewe, walimu wao na jamii nzima ya Marekani.

Barua hiyo imechapishwa wakati kukifanyika uchunguzi wa mwisho wa vitabu vya somo la historia na jiografia kwa ajili ya shule za serikali katika jimbo la California.

Barua hiyo imesema: Tofauti na mtazamo uliomo kwenye vitabu hivyo kuhusu dini nyinginezo, Uislamu unaarifishwa katika kalibu ya vita na utumiaji mabavu. Barua hiyo imesisitiza kwamba mashambulizi ya itikadi zenye taasubi na chuki yaliyoanzia kwenye vyombo vya habari hadi wagombea wa kiti cha rais hayakumuacha salama mtu yeyote na sasa yanawalenga walimu wa shule za Marekani ambao hutambuliwa kuwa vigezo kwa wanafunzi wao.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Taasisi ya Elimu ya California ni jumuiya yenye ushawishi mkubwa sana katika sekta ya elimu nchini Marekani kwa sababu vitabu vya masomo mashule vya taasisi hiyo husambazwa na kufundishwa pia katika majimbo mengine ya Marekani.