May 25, 2024 11:02 UTC
  • Maporomoko ya udongo yaua mamia ya watu New Papua Guinea

Mamia ya watu wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huko Papua New Guinea (PNG).

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Mbunge kutoka mkoa wa kaskazini wa Enga, Aimos Akem akisema kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na majanga hayo ya kimaumbile imeongezeka na kupindukia watu 300.

Amesema nyumba zaidi ya 1,180 zimesombwa na kuharibiwa kikamilifu na maporomoko hayo ya ardhi yaliyotokea jana Ijumaa katika eneo la kaskazini la Maip-Mulitaka.

Kiongozi huyo wa kisiasa amesema maporomoko ya udongo yamefukia mamia ya watu katika vijiji sita vya eneo la Maip-Mulitaka, na kwamba kijiji cha Yambili, yapata kilomita 600 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Port Moresby, kimeharibiwa chote na janga hilo.

Maporomoko ya udongo Papua New Guinea

Habari zaidi zinasema kuwa, maporomoko hayo ya udongo yamefunga pia barabara muhimu ya kuelekea katika mji wa Porgera, wenye migodi ya dhahabu.

Juhudi za uokoaji zinaendelea zikiongozwa na jeshi la Papua New Guinea, huku mataifa mbali mbali yakianza kutuma misaada ya kibidamu katika nchi hiyo ndogo iliyoko kusini magharibi mwa Bahari ya Pasifiki.

Tags