Jun 24, 2024 07:04 UTC
  • Balozi wa utawala wa Kizayuni atimuliwa Colombia

Balozi wa Israel ametimuliwa nchini Colombia baada ya Bogota kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni kutokana na mashambulizi na jinai zisizokwisha za Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa wa Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, Gali Dagan, balozi wa utawala wa Kizayuni nchini Colombia ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwamba ameondoka Bogota mji mkuu wa Colombia.

Vyombo vya habari vya Colombia vimeripoti kwamba "Margarita Menjares", balozi wa nchi hiyo mjini Tel Aviv, pia atarejea nyumbani mwishoni mwa mwezi huu wa Juni pamoja na ujumbe wote wa kidiplomasia wa nchi hiyo ulioko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Balozi wa utawala wa Kizayuni atimulia Colombia

Gustavo Petro, Rais wa Colombia ambaye mwezi Mei alitangaza kuvunja uhusiano na utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kimbari kila siku huko Ghaza, amemkosoa vikali waziri mkuu wa utawala katili wa Israel, Benjamin Netanyahu na kuitaka Colombia iangalie uwezekano wa kujiunga kwenye kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala pandikizi wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Colombia pia ilikatisha ununuzi wake wote wa silaha kutoka kwa utawala wa Kizayuni mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka huu na kutangaza kuwa nchi zote za dunia zinapaswa kumuwekea vikwazo Benjamini Netanyahu waziri mkuu wa Israel anayeongoza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Tags