Umoja wa Ulaya uko tayari kuimarisha ushirikiano na Iran
(last modified Wed, 10 Jul 2024 02:25:32 GMT )
Jul 10, 2024 02:25 UTC
  • Umoja wa Ulaya uko tayari kuimarisha ushirikiano na Iran

Msemaji wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema umoja huo uko tayari kwa ajili ya kupanua wigo wa ushirikiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Nabila Massrali, Msemaji wa Kamisjeni ya Sera za Kigeni ya Umoja wa Ulaya, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Tunazingatia matokeo ya uchaguzi wa rais wa Iran na tunampongeza rais aliyechaguliwa na wananchi, Masoud Pezeshkian." Massrali ameongeza kuwa, umoja huu uko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Iran kwa kuzingatia sera ya maingiliano ya pande mbili. Viongozi wa nchi nyingi za dunia wamepongeza kuchaguliwa kwa rais mpya wa Iran katika siku za hivi karibuni. Ijumaa iliyopita, ikiwa ni katika duru ya 14 ya uchaguzi wa rais, Masoud Pezeshkian alifanikiwa kuwa rais wa tisa wa Iran kwa kupata kura 16,384,403. Uchaguzi huu umefanyika mwaka mmoja mapema kutokana na kufa shahidi marehemu Rais Sayyid Ebrahim Raisi pamoja na viongozi wengine wa Iran katika ajali ya helikopta iliyotokea mwezi Mei kaskazini magharibi mwa nchi.

Nabila Massrali, alikuwa amesema mapema kwamba kipaumbele kikuu cha Umoja wa Ulaya ni "kurahisisha juhudi za kurejea katika utekelezaji kamili wa JCPOA." Umoja wa Ulaya daima umekuwa ukitilia mkazo suala la kupanua uhusiano na Iran kutokana na nafasi muhimu ya kijiografia, kisiasa, kiuchumi na nishati ya nchi hii katika eneo la Mashariki ya Kati na pia nafasi yake muhimu katika kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Pamoja na hayo, hatua ya upande mmoja ya Marekani kujitoa katika mapatano hayo mwezi Mei 2018, kuanzisha vikwazo vya awamu mbili dhidi ya Iran mwezi Agosti na Novemba 2018 na hatimaye hatua ya Rais Donald Trump ya kuutaka Umoja wa Ulaya ujiunge na kampeni yake hiyo dhidi ya Iran, iliufanya umoja huo ukabiliwe na masuala mawili muhimu, yaani kulinda mapatano ya JCPOA na wakati huo huo kukabiliana na mashinikizo ya Washington.

Umoja wa Ulaya uko tayari kupanua ushirikiano na Iran

Kwa mtazamo wa viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya, taasisi hii ya Ulaya katika mazingira ya sasa inabidi kuendelea kushirikiana na Iran kwa ajili ya kuthibitisha uaminifu wake, ili kusaidia kudumisha usalama na uthabiti wa kimataifa. Kwa sababu hiyo, hata baada ya mshirika wake mkuu yaani Marekani, kujiondoa katika mapatano ya JCPOA, Ulaya bado inajiona kuwa inaendelea kujitolea kuyatekeleza. Kinyume na ilivyo Marekani ambayo inadai kuwa Iran haijatekeleza ahadi zake za JCPOA, hivyo haioni mapatano hayo kuwa njia nzuri ya kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran, viongozi wa Ulaya wanaamini kuwa si tu Iran imetekeleza majukumu yake yote ndani ya JCPOA, bali imechukua hatua muhimu katika kuzuia mivutano na migogoro katika eneo na kimataifa.

Kwa hakika, kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, JCPOA ni mfano nzuri wa makubaliano ya pande kadhaa ambao unaweza kutumika kama kielelezo cha utatuzi wa migogoro mingine ya kimataifa. Katika hali hiyo na kwa kuzingatia ushindi wa Masoud Pezeshkian katika uchaguzi wa rais wa Iran na sisitizo lake kuhusu umuhimu wa kushirikiana na nchi zote na kufufuliwa mapatano ya JCPOA, inatarajiwa kwamba mazingira mazuri yamejitokeza kwa ajili ya kuimarisha tena uhusiano wa Tehran na Umoja wa Ulaya. Aidha rais mteule wa Iran ataketi kwenye kiti cha rais wa serikali ya 14 huku uhusiano wa Iran na nchi za eneo na dunia ukizidi kuimarika na inatarajiwa kuwa uhusiano huo utaendelea kuimarika na nchi zote za dunia zikiwemo za Ulaya katika kipindi cha uongozi wa serikali hii.

Kwa kuzingatia kwamba wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Masoud Pezeshkian alisisitiza kuimarisha uhusiano na nchi zote, na kwa kutilia maanani nasaha za mara kwa mara za Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, serikali ya kumi na nne itaendeleza kwa dhati mkakati wa serikali ya Shahid Raisi wa kuimarisha uhusiano na nchi zote za dunia. Hii ni katika hali ambayo kuishi pamoja kwa amani na kuimarisha uhusiano na nchi tofauti daima umekuwa msingi mkuu wa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuhusu suala hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajaribu kudhibiti na kupunguza changamoto zilizopo kwa msingi wa kuwa na mafungamano mazuri ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na nchi nyingine, na wakati huo huo kulinda maslahi ya pande mbili katika mahusiano na nchi hizo.

Tags