Kuingia BRICS katika nyanja mpya za ushirikiano
Sambamba na kufanyika kikao cha St.Petersburg nchini Russia ambapo maspika wa mabunge ya nchi wanachama wa kundi la BRICS walikutana na kujadiliana masuala mbalimbali katika kikao chao cha 10, wasemaji wa wizara za mambo ya nje wa kundi hilo pia walifanya mkutano maalum kando ya kikao hicho ili kuratibu misimamo yao kuhusu sera za kigeni.
Maafisa wakuu wa mabunge ya nchi za BRICS wameelezea wasiwasi wao kuhusu athari mbaya za hatua za mabavu na za upande mmoja ambazo haziheshimu Hati ya Umoja wa Mataifa na kutangaza rasmi upinzani wao dhidi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyotekelezwa na nchi za Magharibi dhidi ya nchi huru duniani.
Katika taarifa ya mwisho ya kikao hicho maspika wa mabunge ya BRICS wameelezea wasiwasi wao kuhusu taathira mbaya za vikwazo hivyo kwa ukuaji wa uchumi, biashara, nishati, afya na usalama wa chakula, haswa katika nchi zinazoendelea. Maspika wa BRICS pia wametangaza kuunga mkono mchakato wa kuwepo biashara ya pande kadhaa, yenye uwazi, adilifu, jumuishi, ya haki, isiyo na ubaguzi na inayozingatia kanuni, ambayo imejikita katika usimamizi wa Shirika la Biashara Duniani.
Mkutano wa 10 wa Mabunge ya BRICS ambao ulifunguliwa rasmi kwa hotuba ya Rais Vladimir Putin wa Rushia ulimalizika huko St.Petersburg siku ya Ijumaa, Julai 22. Mada ya mkutano huo ilihusu jukumu la mabunge katika kuimarisha ushirikiano wa pande kadhaa kwa ajili ya maendeleo na usalama duniani.

Nafasi ya mabunge katika kuimarisha ufanisi wa mfumo wa mahusiano ya kimataifa na demokrasia, nafasi ya mabunge katika biashara ya kimataifa na jinsi ya kuondokana na vitisho vinavyosababishwa na migogoro ya kimataifa, pamoja na ushirikiano wa kibinadamu na kiutamaduni kati ya mabunge ni masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho.
Wabunge wa nchi za BRICS wanasisitiza umuhimu wa kuimarishwa usalama wa kiuchumi na kifedha, kufikiwa malengo ya maendeleo ya kitaifa ya nchi za BRICS na mkakati wa ushirikiano wa kiuchumi wa BRICS kufikia mwaka 2025. Ikiwa ni mwenyekiti wa mzunguko wa kundi la BRICS, Russia itakuwa mwenyeji wa shughuli na vikao karibu 250 vya kundi hilo mwaka huu.
Katika upande wa pili, wasemaji wa taasisi za kidiplomasia za nchi wanachama wa BRICS walikutana pia katika kikao cha St. Petersburg na kujadiliana kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha misimamo ya kimataifa ya BRICS na kuunda jukwaa la pamoja la habari.
Akizungumza katika kikao hicho, Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitoa hotuba akifafanua misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala kama vile hatua ya pamoja ya vyombo vya habari vya nchi wanachama wa BRICS katika kuimarisha msimamo wa kimataifa wa kundi hili kwa kutumia uwezo wa diplomasia ya kidijitali na akili mnemba katika diplomasia ya umma na sera za kigeni, na kupambana na mtiririko wa habari bandia na za kupotosha.
Umuhimu wa uanachama wa Iran katika kundi la BRICS unadhihirika wazi tunapotilia maanani kwamba kati ya jumla ya mabadilishano ya biashara yenye thamani ya takriban dola bilioni 114, mabadilishano ya karibu dola bilioni 68 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya biashara hiyo, yalifanyika kati yake na nchi wanachama wa BRICS. Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa wanachama wa BRICS wanaojumuisha nchi zinazoinukia kiuchumi, wanafuatilia juhudi za kuimarisha ushawishi wao wa kiuchumi na kijiografia katika ngazi za kimataifa katika hali ambayo uchumi wao katika miaka miwili iliyopita umefikia asilimia 29 ya uchumi wote wa dunia, ambapo unakaribia ule wa asilimia 43 wa kundi la G7.

Kundi la G7 ambalo linaundwa na nchi za Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, lilimiliki asilimia 43 ya uchumi wa dunia mwaka 2000, ambapo idadi hiyo haijabadilika kufikia sasa. Hii ni katika hali ambayo hisa ya BRICS imeongezeka kutoka asilimia 18 mwaka 2000 hadi asilimia 29 mwaka uliopita wa 2023.
Data nyingine ya kuzingatia ni ulinganisho wa nafasi ya BRICS na Marekani katika biashara ya dunia. Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa wakati mauzo ya nje ya Marekani yamekuwa kati ya asilimia 8 hadi 9 tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2004, hali hiyo kwa nchi wanachama wa BRICS imeongezeka kutoka asilimia 13 hadi asilimia 23.
Takwimu hizi zinaonyesha ruwaza ya wazi ya mustakbali wa BRICS, na kama ilivyoonekana katika mkutano wa St. Petersburg, kwa kupita wakati na katika kivuli cha juhudi na mapendekezo ya Iran, wigo wa shughuli za kundi hili umekuwa ukiimarika siku baada ya siku.