Rais wa Brazil: Dunia isinyamazie kimya mauaji ya Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i114102-rais_wa_brazil_dunia_isinyamazie_kimya_mauaji_ya_wapalestina_gaza
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-07-16T02:54:11+00:00 )
Jul 16, 2024 02:54 UTC
  • Rais wa Brazil: Dunia isinyamazie kimya mauaji ya Wapalestina Gaza

Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Da Silva alinukuliwa akisema hayo na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar jana Jumatatu na kuongeza kuwa, "Mashambulizi ya mabomu ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza hayakubaliki."

Ameeleza bayana kuwa, utawala huo unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, na kwamba Umoja wa Mataifa na taasisi zake kama Baraza la Usalama lazima ziwe na ujasiri wa kuhakikisha kuwa inaundwa nchi huru ya Palestina.

Da Silva amesema ukiukaji wa kila siku wa sheria na haki za binadamu ambao umegharimu maisha ya maelfu ya raia wasio na hatia huko Gaza, iliisukuma nchi hiyo kuunga mkono uamuzi wa Afrika Kusini wa kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil

Amebainisha kuwa, haki ya kujihami inayodaiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza imegeuka na kuwa haki ya kulipiza kisasi katika kivuli cha ukiukwaji wa kila siku wa sheria na haki binadamu.

Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amekuwa akivifananisha vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya "Holocaust" yanayodaiwa kufanywa na Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mei mwaka huu, Brazil ilimrejesha nyumbani balozi wake wa Israel kulalamikia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambayo yamepelekea Wapalestina zaidi ya 38,000 kuuawa shahidi tangu Oktoba, 2023.