Umoja wa Ulaya wazitaka nchi wanachama kujiandaa na wimbi la MPOX
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115322-umoja_wa_ulaya_wazitaka_nchi_wanachama_kujiandaa_na_wimbi_la_mpox
Shirika la afya la Umoja wa Ulaya limezitaka nchi wanachama wa umoja huo kujiandaa na uwezekano wa wagonjwa zaidi wa virusi vya homa ya MPOX.
(last modified 2024-08-17T03:40:16+00:00 )
Aug 17, 2024 03:40 UTC
  • Umoja wa Ulaya wazitaka nchi wanachama kujiandaa na wimbi la MPOX

Shirika la afya la Umoja wa Ulaya limezitaka nchi wanachama wa umoja huo kujiandaa na uwezekano wa wagonjwa zaidi wa virusi vya homa ya MPOX.

Kituo cha Ulaya cha kuzuia na kudhibiti magonjwa ECDC kimesema hali ya hatari ndani ya Umoja wa Ulaya bado iko chini.

Kituo hicho hata hivyo kimetoa mwito kwa mamlaka za afya ya umma ndani ya Umoja wa ulaya kuwa macho na kuuhamasisha umma juu ya ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha ECDC Pamela Rendi-Wagner amesema katika taarifa kuwa, Ulaya inapaswa kujiandaa kwa wagonjwa zaidi hasa aina mpya ya virusi vya MPOX vya clade 1.

Baada ya kuua mamia ya watu barani Afrika, sasa umonjwa wa Mpox umeripotiwa kuingia barani Ulaya hususan Sweden.

Ni baada ya Sweden kutangaza kisa cha kwanza cha ugonjwa huo ambao umeua watu 548 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni ishara ya kuenea kwake nje ya bara la Afrika.

 

Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatano iliyopita lilitangaza mlipuko wa Mpox nchini DRC na nchi nyingine za Afrika kama "dharura ya afya duniani".

Wakati huo huo, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika kimetangaza "dharura ya afya ya umma", kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, kuhusu mlipuko wa Mpox unaokua katika bara hilo, na kutoa "wito wa kuchukuliwa hatua" za kukomesha msambao wake.

Jumla ya visa 38,465 vya ugonjwa huu, ambao zamani ulijulikana kama Homa ya nyani, vimerekodiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mwezi Januari 2022, pamoja na vifo 1,456, na ongezeko la 160% la kesi mnamo mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kulingana na data zilizochapishwa wiki iliyopita na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, Africa CDC.