Onyo la Guterres kuhusu mporomoko wa ubinadamu huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115378-onyo_la_guterres_kuhusu_mporomoko_wa_ubinadamu_huko_gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonya kwamba eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina liko katika "mporomoko huru wa ubinadamu". Guterres ameyasema hayo akizungumzia hali mbaya na mgogoro mkubwa unaowasumbua na kuwatesa wakazi wa eneo hilo.
(last modified 2024-08-18T22:48:13+00:00 )
Aug 18, 2024 22:48 UTC
  • Onyo la Guterres kuhusu mporomoko wa ubinadamu huko Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonya kwamba eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina liko katika "mporomoko huru wa ubinadamu". Guterres ameyasema hayo akizungumzia hali mbaya na mgogoro mkubwa unaowasumbua na kuwatesa wakazi wa eneo hilo.

Akieleza kuwa hali ya Wapalestina huko Gaza inazidi kuwa mbaya kila kukicha, Guterres ameiomba jamii ya kimataifa kuchukua hatua ili kuzuia ongezeko la mateso kwa watu wa Gaza.

Miezi 11 imepita tangu Israel ianze kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Mbali na kuuliwa shahidi zaidi ya Wapalestina elfu 40 na wengine zaidi ya elfu 93 kujeruhiwa, magonjwa mbalimbali yanaenea kwa kasi huko Gaza na yanatishia maisha ya raia wasio na ulinzi. Katika wiki za hivi karibuni, virusi vya polio vimesambaa kati ya watu, haswa watoto, na sababu kuu ni maji machafu. Antonio Guterres ametangaza kuwa virusi vya polio vimegunduliwa katika sampuli za maji taka huko Gaza katika wiki za hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameonya kwamba iwapo virusi hivyo havitadhibitiwa, vinaweza kuwa na matokeo mabaya sio tu kwa watoto wa Palestina, bali kwa eneo zima la Magharibi mwa Asia. Guterres ameiomba jamii ya kimataifa kupigana vita na polio na kuvishinda virusi hivyo hatari kwa afya badala ya kupigana vita na watu. Guterres amesisitiza kuwa kuendelea kwa vita kunazuia utekelezaji wa kampeni ya kutoa chanjo, na suala hili liko juu ya siasa; hivyo pande zote zinalazimika kushirikiana katika kupambana na polio na kuzuia athari zake mbaya kwa watoto wa Palestina huko Gaza na nchi jirani.

Antonio Guterres

Dr Margaret Harris, msemaji wa Shirika la Afya Duniani, pia amesema kuwa dalili za kwanza za mlipuko wa polio zimeonekana huko Gaza. Amesema Shirika la Afya Duniani linatoa wito wa kufunguliwa tena kivuko cha Rafah haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuingizwa Gaza chanjo na dawa ambazo ni muhimu kwa maisha ya binadamu.

Awali, Ayadil Saparkov, mkuu wa timu ya dharura ya afya katika Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, amesema kuwa hatari ya kuenea virusi vya polio huko Gaza iko juu kutokana na hali mbaya ya kiafya na maji machafu ya kunywa. Amesema kuwa virusi vya polio sasa vimetoka kwenye maji taka na vinasambaa kote Gaza.

Gaza

Mbali na mlipuko wa magonjwa, ikiwa ni pamoja na polio, watu wa Gaza pia wanasumbuliwa na njaa inayotishia maisha ya watu hasa watoto na wanawake.

Wakati huo huo ripoti zinasema utawala wa Kizayuni wa Israel umezuia misaada ya kibinadamu kutumwa Gaza kwa muda wa siku 100 zilizopita. Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imetoa taarifa ikitangaza kuwa: Jeshi la Kizayuni limefunga kivuko cha mpaka kati ya Palestina na Misri kwa muda wa siku 100 zilizopita na kuzuia kuingizwa aina zote za misaada katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu, dawa, misaada ya kibinadamu na hata timu za madaktari. Idara hiyo imesisitiza kuwa, mienendo hiyo ya jeshi la Kizayuni inaambatana na ongezeko lisilo na kifani la maafa ya binadamu katika nyanja zote za maisha ya watu wa Ukanda wa Gaza, na ni jinai zinazokiuka sheria za kimataifa, haki za binadamu na makubaliano yote ya kimataifa.

Watoto wa Gaza

Ni kwa kuzingatia hali hii mbaya, ndipo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akazungumzia suala la mporomoko huru wa ubinadamu huko Gaza. Hali hii mbaya ni ushahidi tosha wa kushindwa kimaadili kwa jamii ya kimataifa huko Gaza na Palestina kwa ujumla.