Maandamano ya kulaani jinai za Israel yafanyika tena nchini Ujerumani
Maelfu ya wananchi wa mji mkuu wa Ujerumani Berlin wameandamana tena wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wapalestina hususan wa Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu sambamba na kulaani jinaii za Israel wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina.
Kadhalika waandamanaji hao wakiwa na bendera ya Palestina wamesisitiza udharura wa kusitishwa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na kukombolewa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Isarel.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa, sambamba kuanza kurejea wanafunzi katika vyuo vikuu vya nchi hiyo, maafisa wa vyuo hivyo kote nchini humo wanajiandaa kukabiliana na wimbi jipya la maandamano ya wanachuo dhidi ya utawala katili wa Israel.

Kufungwa vyuo vikuu na likizo ya majira ya kiangazi nchini Mrekani kulikatiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo hivyo dhidi ya ukatili wa Israel katika vita vya Gaza, na wakati huo huo viliwapa wanafunzi waliokuwa wakiandamana, maafisa wa elimu ya juu wa Marekani marais wa vyuo vikuu na wasimamizi wao, fursa ya kupanga hatua zao za baadaye katika majira ya mapukutiko.
Kwa sasa, maafisa wa vyuo vikuu vya Marekani wanajiandaa kukabiliana na harakati mpya na maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu dhidi ya vita Israel huko Gaza. Baadhi ya vyuo hivyo vinapanga kutekeleza sheria mpya ili kubana maandamano ya wanachuo kama yale yaliyovikumba vyuo vikuu vya Marekani majira ya machipuo. Baadhi ya sheria mpya zilizopitishwa na vyuo hivyo ni pamoja na kupiga marufuku kuweka mahema ya waandamanaji, kuweka kikomo cha muda wa maandamano, kuruhusu maandamano kufanyika katika maeneo maalumu tu, na kuzuia maandamano yasifanyike katika maeneo yenye majengo ya elimu au ya utawala ya vyuo vikuu.