The Independent: 92% ya Waislamu wa Uingereza hawana amani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115386-the_independent_92_ya_waislamu_wa_uingereza_hawana_amani
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kuchapishwa na gazeti la The Independent la Uingereza unaonyesha kuwa, asilimia 92 ya Waislamu wa nchi hiyo hawahisi kuwa na amani.
(last modified 2024-08-18T23:27:53+00:00 )
Aug 18, 2024 23:27 UTC
  • The Independent: 92% ya Waislamu wa Uingereza hawana amani

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kuchapishwa na gazeti la The Independent la Uingereza unaonyesha kuwa, asilimia 92 ya Waislamu wa nchi hiyo hawahisi kuwa na amani.

Uchunguzi huo wa maoni unaeleza kuwa, asilimiia 92 ya Waislamu wanahisi kutokuwa amani kabisa ya kuishi nchini Uingereza.

Kulingana na uchunguzi wa maoni uliofanywa na  shirika la Muslim Census ambalo hukusanya data kuhusu Waislamu na watu wa jamii za waliowachache ni kuwa, vurugu na ghasia za mrengo wa kulia wenye misimamo mikali zimekuwa na athari mbaya kwa Waislamu na kuwafanya wajisikie kutokuwa amani hata kidogo nchini Uingereza.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanatolewa katika hali ambayo, hivi sasa Uingereza inashuhudia kuongezeka wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na Wislamu lililoibuliwa na watu wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali.

Maandamano ya makundi yenye chuki dhidi ya Uislamu

Ghasia kubwa zilianza katika aghalabu ya miji ya Uingereza mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, baada ya barobaro mmoja mwenye umri wa miaka 17 kushambulia hafla iliyokuwa ikifanyika katika shule moja ya watoto katika mji wa Southport.

Watoto watatu waliuawa katika hujuma hiyo. Watoto wengine kadhaa na watu wazima wawili waliokuwa wamejeuhiwa vibaya, walipelekwa hospitali kufuatia shambulio hilo la kisu.

Mara tu baada ya tukio hilo, habari za uongo zilichapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza kwamba barobaro huyo alikuwa mhajiri Mwislamu. Wafuasi wenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia walitumia vibaya taarifa hiyo ya uongo kama kisingizio cha kuanza kuwashambulia Waislamu, vituo na maneo yao ya ibada. Hata hivyo ilibainika baadaye kwamba mtu aliyehusika na shambulizi hilo si Muislamu wala mhajiri, na kwamba ni mzaliwa wa Uingereza.