OCHA: Wafanyakazi 280 wa huduma za kibinadamu waliuawa mwaka 2023
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa, wafanyakazi 280 wa utoaji huduma za kibinadamu waliuawa kwenye mataifa 33 katika mwaka uliiopiita wa 2023.
Hayo yameelezwa huku dunia ikiadhimisha Siku ya Huduma za Kibinaadamu. Umoja wa Mataifa unasema kuwa, wafanyakazi wa huduma za kibinadamu waliouawa kwenye maeneo yenye migogoro duniani mwaka jana ilivunja rikodi, lakini mwaka huu huenda ukawa mbaya zaidi.
Kaimu Mratibu wa Huduma za Dharura wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya, amesema, vifo vingi zaidi vya mwaka jana vilitokea kwenye Ukanda wa Gaza huko Palestiina katika miezi mitatu ya mwanzo ya mashambulizi ya Israel kwenye ukanda huo yaliyoanza mwezi Oktoba.
Hili ni ongezeko la asilimia 137 na zaidi ya mara mbili ya vile hali ilivyokuwa mwaka 2022, ambapo waliouawa walikuwa 118.
Sudani Kusini, iliyokumbwa na ghasia za kiraia na mapigano ya kikabila, na Sudan, ambako vita kati ya majenerali wawili hasimu vimeshamiri tangu mwezi Aprili 2023, ni mizozo mingine miwili mibaya zaidi kwa wahudumu wa masuala ya kibinadamu, ambapo kuliripotiwa vifo 34 na 25 kwa utaratibu. Aidha katika maeneo 10 yanayoongoza kwa uhalifu huo ni Israel na Syria (vifo saba kila moja), Ethiopia na Ukraine (vifo sita kila moja), Somalia (vifo vitano), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Myanmar vifo vinne kila moja.
Kila mwaka, Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani mnamo Agosti 19 kukumbuka shambulio katika makao makuu yake huko Baghdad mnamo mwaka 2003.