Jibu la China kwa waraka wa mkakati wa nyuklia wa Marekani
Baada ya kutangazwa habari ya kuthibitishwa waraka wa siri wa kistratijia wa nyuklia wa Marekani wa kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa upanuzi wa haraka wa silaha za nyuklia za China, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hii imesema waraka huo ni kisingizio tu cha kupanua mpango wa silaha za nyuklia wa Marekani.
Katika kujibu ripoti hiyo iliyochapishwa na gazeti la New York Times, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesisitiza kuwa Marekani ndiyo chanzo kikubwa cha hatari za kimkakati za nyuklia duniani, kwa sababu kwa kuendeleza nadharia ya tishio la nyuklia la China, inataka kupata kisingizio cha kupanua maghala yake ya silaha za nyuklia kwa maslahi yake ya kimkakati.
Tokea wakati wa uongozi wa Barack Obama, sera ya Marekani ilibadilika kuelekea zaidi upande wa kukabiliana na China. Wakati huo Marekani ilituma majeshi yake kwenye bahari zilizo jirani na China kwa lengo la kuizingira kijeshi. Wakati wa urais wa Donald Trump, sera za mashinikizo za Washington dhidi ya China ziliongezeka ambapo kulishuhudiwa ongezeko kubwa la chuki dhidi ya China au Sinophobia hasa katika uga wa kiuchumi. Hivi sasa, sera ya Sinophobia ya Marekani imepanuliwa kupitia suala la nyuklia.
Li Van Ti, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: "Moja ya njia za Marekani kukabiliana na China ni kujaribu kuunda muungano dhidi ya Beijing, ambapo suala la nguvu ya nyuklia ya China linaibuliwa. Maoni ya umma nchini Korea Kusini na Japan ni dhidi ya uwepo wa Marekani katika nchi yao na kwa hiyo Marekani inajaribu kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo kwa kueneza hofu na chuki dhidi ya China."
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la New York Times, likiwanukuu maafisa kadhaa wa Pentagon na Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani, Joe Biden, ameidhinisha waraka wa siri kuhusu mkakati wa nyuklia kwa lengo la kutishia Russia China na Korea Kaskazini.
Waraka huo unaojulikana kama Mwongozo wa Matumizi ya Silaha za Nyuklia, uliidhinishwa mwezi Machi na kuashiria mara ya kwanza doktirini ya nyuklia ya Marekani ya kuzingatia uwezo wa nyuklia wa Beijing. Duru nyingi za kisiasa na kijeshi duniani zinaamini kwamba serikali ya Marekani, ili kuwakinaisha wananchi kuhusu sera zake za kueneza silaha za nyuklia, inadai kuwa China ni tishio la nyuklia.
Ukweli ni kwamba uhai wa Marekani kimataifa hutegemea vurugu na ukosefu wa usalama, na nchi hii inajaribu kuendeleza nguvu yake ya kimataifa kwa kuchochea migogoro na kuzidisha ukosefu wa usalama duniani. Kwa hiyo, jumuiya ya kimataifa inafahamu kikamilifu madai ya uongo ya Marekani.
Kwa msingio huo, Washington inazidi kuinua kiwango cha tishio cha China. Ukweli ni kwamba Marekani ina rekodi mbaya zaidi ya jinai dhidi ya binadamu wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia wakati ilipodondosha mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki. Jambo la kusikitisha ni kuwa nchi hiyo ya kibeberu ya Magharibi daima hujaribu kuficha shughuli zake haribifu kwa kudai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu.