Russia kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na ugonjwa wa mpox
Shirika la Russia la Rospotrebnadzor litazipatia nchi za Afrika vifaa vya kupima na kutambua virusi vya mpox, ambavyo zamani viliitwa monkeypox.
Kulingana na RT, wataalamu kutoka Rospotrebnadzor pia wamekuwa wakifanya kozi wiki hii juu ya kuzuia na utambuzi wa maambukizi ya mpox katika Jamhuri ya Kongo
Jamhuri ya Kongo imeonyesha nia ya kuendelea kupata vifaa vya Russia vya kupima mpox na kuimarisha ushirikiano na Rospotrebnadzor kwa jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo. Kulingana na taarifa hiyo, Rospotrebnadzor inapanga "kusaidia washirika wa kimataifa ...[na] itatoa huduma za kukabiliana na kirusi cha mpox kwa nchi zingine za Afrika."
Rospotrebnadzor hapo awali ilitangaza kwamba imetengeneza chanjo ya kuzuia mpox. Shirika hilo pia linafanya utafiti wa kisayansi unaolenga kuzuia, matibabu, na utambuzi wa vimelea vya ugonjwa huo.
Ongezeko la hivi majuzi la visa vya mpox katika mataifa mengi ya Afrika lilisababisha Shirika la Afya Duniani WHO kutangaza dharura ya afya ya kimataifa wiki iliyopita.
Kulingana na shirika hilo, zaidi ya kesi 14,000 na vifo 524 vimeripotiwa ulimwenguni kote mwaka huu, na kupita jumla ya vifo vya mwaka jana. Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, kuumwa na misuli, maumivu ya mgongo, nodi za limfu zilizovimba, kusikia baridi, na uchovu, na wale wanaougua hupata vidonda vya kipekee katika ngozi.