UN: Moshi wakati wa kupika uliua watu milioni 3.1 mwaka 2021
Moshi wakati wa kupika majumbani ulisababisha vifo vya mapema vya watu milioni 3.1 mnamo 2021 ambapo idadi kubwa ya waliofariki ni kutoka bara la Afrika.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, (UNEP) ambayo imesema kuwa mabilioni ya watu katika ulimwengu unaoendelea, hasa watoto na wanawake, muda wa chakula huanza kwa kuwasha jiko la mafuta ya taa, kuwasha jiko la mkaa au kuwasha moto wa magogo.
Martina Otto, Mkuu wa Sekretarieti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, (UNEP) amesema uchafuzi wa hewa nyumbani ni mojawapo ya matishio makubwa zaidi ya afya ya umma duniani na ni hatari kwa Watoto.
Taarifa hiyo ya UNEP iliyosambazwa jana tarehe 7 Septemba, ilisadifiana na Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa ajili ya anga ya buluu na huadhimishwa ili kuongeza ufahamu kuhusu hatari za uchafuzi wa hewa.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa mwaka 2021 kati ya watu milioni 3.1 walipoteza maisha kutokana na uchafuzi wa hewa wa nyumbani ambapo watoto 237,000 walio chini ya miaka mitano walikuwa wahanga. Uchafuzi wa hewa wa nyumbani pia huathiri wanawake kwa njia isiyo sawa, kwani mara nyingi wanapika. Katika Afrika, wanawake na watoto ni asilimia 60 ya vifo vya mapema vinavyohusiana na kuvuta moshi na uchafuzi wa hewa wa nyumbani.
Serikali duniani zinahimizwa kuwezesha wananchi kupata nishati safi ya kupika. Ufafanuzi wa kawaida wa upikaji safi ni aina yoyote ya mafuta na jiko ambavo vinakidhi miongozo ya Shirika la Afya Dunaini kwa ubora wa hewa ya ndani ya nyumba. Hiyo kwa kawaida hujumuisha majiko yanayoendeshwa na umeme, gesi asilia, ethanoli na gesi ya kioevu ya petroli, ambayo ni safi. Inaweza pia kujumuisha majiko yanayotumia mkaa wenye ufanisi wa juu ambao hutoa moshi mdogo kuliko majiko ya jadi.