Sep 15, 2024 11:41 UTC
  • Diosdado Cabello
    Diosdado Cabello

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Venezuela imetangaza kuwa imezima mpango wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) wa kutaka kumuua rais wa nchi hiyo, Nicolás Maduro.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Venezuela imesema kuwa, raia 6 wa kigeni, wakiwemo raia 3 wa Marekani, 2 wa Uhispania na raia mmoja wa Jamhuri ya Czech, wamekamatwa nchini humo kwa tuhuma  za kuhusika na jaribio hilo.

Diosdado Cabello, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela, ametangaza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya nchi hiyo kwamba ilipangwa kuwa raia hao wa kigeni wangeshiriki katika mpango wa CIA wa kupindua serikali ya Venezuela na kuua viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa nchi hiyo, akiwemo Rais Maduro. 

Akizungumzia silaha zilizogunduliwa ambazo ziliingizwa nchini Venezuela kinyume cha sheria kutoka Marekani, Cabello amesema kuwa silaha hizo zilikamatwa kutoka kwa kundi jingine la maajenti wa shirika la ujasusi la Marekani waliohusika katika njama ya kumuua Maduro.

Maduro na Diosdado Cabello

Wazara wa Mambo ya Ndani wa Venezuela amesema kwamba, mmoja wa raia wa Marekani waliokamatwa anayejulikana kwa jina  la "Wilbert Joseph Castanda Gomez" ni askari wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, na kuongeza kuwa, Gomez ana historia ya kuhudumu katika nchi za Afghanistan, Iraq na Colombia.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kukamatwa kwa mwanajeshi wa zamani wa nchi hiyo nchini Venezuela.