Waislamu wapendekeza mgombea wa tatu katika uchaguzi wa rais Marekani
Licha ya mgombea urais wa chama cha Democratic, Kamala Harris, kuwa na nafasi nzuri zaidi na kumtimulia kivumbi mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump, katika kura za maoni za hivi karibuni, kura za Waislamu wa Marekani sasa zimeweka kipaumbele kwa mgombea wa Chama cha Kijani, Jill Stein, ambaye anaunga mkono waziwazi kadhia ya mapambano ya Palestina na amemchagua Mwislamu kushika nafasi ya makamu wa rais iwapo atashinda.
Stein ameongoza kwa tofauti kubwa dhidi ya Harris na Trump katika majimbo 3 kati ya 7 yaliyoelezwa kuwa ya "maamuzi" katika uchaguzi wa rais licha ya kufifia kwa nafasi yake ya kushinda uchaguzi huo kutokana na udhibiti wa kihistoria wa vyama vya Democratic na Republican katika mbio za kuelekeka Ikulu ya White House.
Kudhihiri kwa mgombea huyo huru kunazusha mkanganyiko katika misimamo ya wapiga kura Waislamu, ambao wamegawanyika kati ya wale wanaoona kwamba, kumpigia kura Stein ni kupoteza bure kura hizo, na wale wanaoamni kwamba kuna idharura wa kuwatia adabu Harris na Trump kutokana na msimamo wao juu ya vita katika Ukanda wa Gaza.
Waislamu katika majimbo muhimu ya Marekani walimpa kura zao Rais wa sasa, Joe Biden, na walikuwa na nafasi kubwa katika kuingia kwake Ikulu ya White Hose, lakini hakuwajali kivitendo wakati vilipoanza vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.
Idadi ya wapiga kura Waislamu inazidi kidogo kura milioni moja, lakini wanasambaa katika majimbo ambayo yana umuhimu mkubwa katika Electoral College, ambacho ndicho chombo chenye uamuzi wa mwisho wa nani atashinda na kuingia Ikulu ya Rais.