Pager zilizotumika katika ugaidi nchini Lebanon 'zilitengenezwa Hungary'
Kampuni ya Taiwan Gold Apollo inasema kwamba pager zilizotumiwa katika shambulio la kigaidi la Israel dhidi ya Lebanon siku ya Jumanne zilitengenezwa na kampuni ya Hungary.
Kampuni hiyo ilitoa matamshi hayo katika taarifa Jumatano, na kubainisha kampuni hiyo ijulakanayo kama BAC Consulting KFT yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Hungary Budapest, ilipata idhini ya kutumia jina la Gold Apollo kwenye pager hizo.
Pager ni kifaa cha mawasiliano kisichotumia waya ambacho hupokea na kuonesha jumbe za alphanumeric au sauti
Taarifa hiyo ilisema, "Kulingana na makubaliano ya ushirikiano, tumeidhinisha BAC kutumia chapa ya biashara yetu kwa mauzo ya bidhaa katika maeneo yaliyoteuliwa, lakini muundo na utengenezaji wa bidhaa ni jukumu la BAC pekee."
Kampuni hiyo pia iliondoa tangazo linalobainisha sifa za pager hiyo kutoka kwenye tovuti yake baada ya shambulio hilo.
Wizara ya Masuala ya Kiuchumi ya kisiwa hicho kinachojitawala pia imejaribu kusema kuwa kampuni hiyo ya Gold Apollo haikuhusika na shambulizi hilo
Aidha imedai kuwa kampuni hiyo imesafirisha pager 260,000 hasa kwa nchi za Ulaya na Amerika kuanzia mwanzoni mwa 2022 hadi Agosti mwaka huu, na ilidai kuwa haina rekodi za mauzo ya moja kwa moja ya vifaa hivyo kwenda Lebanon.
Siku ya Jumanne, vilipuzi vilivyotegwa kwenye pager za AR-924 vililipuka katika maeneo mbalimbali nchini Lebanon kwa wakati mmoja, na kuua watu wasiopungua 12, akiwemo msichana wa miaka 8, na kujeruhi karibu wengine 3,000.
Kulingana na Waziri wa Afya wa Lebanon Firas Abiad, wengi wa waliojeruhiwa walikuwa wamepata majeraha mabaya machoni na wengine kukatwa miguu na mikono.
Serikali ya Lebanon na harakati ya muqawama ya Hizbullah ya nchi hiyo imeutalumu utawala ghasibu wa Israel kwa hujuma hiyo ya kigaidi na kuuonya utawala huo kuwa utapata jibu kali kwa ukatili huo.