Japan yaamuru watu kuhama makazi yao kutokana na tishio la mafuriko
https://parstoday.ir/sw/news/world-i116624-japan_yaamuru_watu_kuhama_makazi_yao_kutokana_na_tishio_la_mafuriko
Serikali ya Japan imetoa amri ya kuhama watu kutoka katika makazi yao katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ikiwa ni indhari ya tishio la mafuriko yanayoijongea nchi hiyo ya bara Asia.
(last modified 2024-09-21T23:27:41+00:00 )
Sep 21, 2024 23:27 UTC
  • Japan yaamuru watu kuhama makazi yao kutokana na tishio la mafuriko

Serikali ya Japan imetoa amri ya kuhama watu kutoka katika makazi yao katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ikiwa ni indhari ya tishio la mafuriko yanayoijongea nchi hiyo ya bara Asia.

Ripoti zinasema kuwa, makumi ya maelfu ya watu katika miji minne katikati mwa Japan wametakiwa kuhama baada ya watabiri wa hali ya hewa kuonya kuhusu mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Takriban watu 18,000 katika jiji la Wajima na wengine 12,000 huko Suzu wametakiwa kutafuta hifadhi katika mkoa wa Ishikawa, kisiwa cha Honshu.

Kadhalika wakaazi wengine 16,000 katika wilaya ya Niigata na Yamagata kaskazini mwa Ishikawa pia wametakiwa kuhama, shirika la habari la AFP lilisema.

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan imetoa dharura ya mvua kubwa - kiwango cha juu zaidi cha tahadhari – katika sehemu za eneo hilo.

Shirika la utangazaji la umma la Japan NHK lilinukuu maafisa wa serikali wakisema kuwa, mito 12 imevunja kingo zake na kusababisha mafuriko makubwa.

Aidha shirika hilo la utangazaji la Japan limerushwa hewani picha na video zinazoonyesha mtaa mzima wa Wajima ukiwa umezama chini ya maji.

Mito mitatu huko Ishikawa imefurika katika jamii za karibu, afisa wa eneo hilo ameziambiia duru za habari.

Katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko huduuma muhimu kama umeme na mawasiliano hazipatikani.