Russia yatahadharisha kuhusu athari za matukio ya karibuni huko Lebanon
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu matokeo ya matukio ya karibuni huko Lebanon katika mfumo wa kimataifa.
Dmitry Poliyansky ameeleza kuwa milipuko ya vifaa vya pager huko Lebanon imeibua maswali mengi ikiwa ni pamoja na kuhusu usalama wa taarifa na kusema: Uchunguzi unapasa kufanyika kuhusu athari za hujuma hiyo na kisha kutolewa mapendekezo ya lazima.
Vasily Nebenzya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa pia amesema kuhusu milipuko na mashambulizi ya kigaidi huko Lebanon kuwa kilichotokea ni kushadidisha mivutano katika eneo la Asia Magharibi katika mwelekeo mpya wa teknolojia ya kisasa.
Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia amesema, kilichotokea Lebanon ni hatua ya kigaidi na ya kikatili na jitihada zenye lengo la kuchochea vita vikubwa.
Utawala ghasibu wa Israel pia umewauwa shahidi raia wasiopungua 37 wa Lebanon na kuwajeruhi wengine zaidi ya 4,000 katika operesheni za kigaidi za Jumanne na Jumatano Septemba 17 na 18 mwaka huu kwa kulipua maelfu ya vifaa vya pager; mifumo ya mawasiliano isiyotumia nyaya.
Nchi na taasisi nyingi za kimataifa zimelaani milipuko ya karibuni huko Lebanon na kusisitiza ulazima wa kupunguza mivutano katika eneo.