Kwa sababu ya keffiyeh ya Kipalestina...mwandishi maarufu akataa tuzo ya Marekani
-
Jhumpa Lahiri
Mwandishi aliyeshinda Tuzo ya Pulitzer, Jhumpa Lahiri, amekataa kupokea tuzo ya Jumba la Makumbusho la Noguchi la New York City huko Marekani baada ya kuwafuta kazi wafanyakazi watatu kwa kuvaa skafu za keffiyeh, ambayo ni nembo ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina wanaoendelea kuuawa na majeshi ya Israel.
Jumba hilo la makumbusho lilitangaza jana, Jumatano, kwamba mwandishi huyo wa Kimarekani mwenye asili ya India amekataa kupokea Tuzo ya Isamu Noguchi ya 2024, (Isamu Noguchi Award) "akipinga kile kilichoitwa sera ya kusasisha kanuni za mavazi."
Watu katika pembe mbalimbali za dunia, wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kukomesha vita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina wakiwa na skafu au keffiyeh kichwani, ambayo ni ishara ya kujitawala kwa Wapalestina. Kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela pia alionekana akivaa skafu hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Paletina mara nyingi.
Watetezi na waungaji mkono wa utawala katili wa Israel wanapinga vikali suala hilo na wanawapachika wavaaji wake tuhuma mbalimbali zikiwemo za ugaidi na misimamo mikali.
Jhumpa Lahiri, ambaye alishinda Tuzo ya Pulitzer mwaka wa 2000 kwa kitabu chake, Interpreter of Maladies, alikuwa mmoja wa maelfu ya wasomi ambao walitia saini barua mwezi Mei ambayo ilitumwa kwa marais wa vyuo vikuu nchini Marekani, wakitangaza mshikamano wako na maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu dhidi ya vita vya Israel na mauaji ya kimbari ya utawala huo huko Gaza.
Taasisi mbalimbali za Marekani zimekuwa zikiwafukuza kazi au kuwachukulia hatua kali watu wote wanaopinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina na sasa Lebanon.
Mwezi Novemba mwaka jana, wanafunzi watatu wenye asili ya Kipalestina, wawili miongoni mwao wakiwa wamevaa keffiyeh, walipigwa risasi katika shambulizi katika jimbo la Vermont nchini Marekani.
Mwezi Mei mwaka huu pia, hospitali ya jiji la New York ilimfukuza kazi muuguzi Mmarekani baada ya kutaja vita vya Israel huko Gaza kuwa "mauaji ya halaiki".