Ulaya ni muhali kuafikiana kuhusu vita dhidi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i116820-ulaya_ni_muhali_kuafikiana_kuhusu_vita_dhidi_ya_russia
Wakati Rais wa Russia ameonya kuhusu madhara yasiyotabirika ya kutumiwa silaha za nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo, imedhihirika wazi kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuchukua uamuzi wa pamoja wa kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za Magharibi kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Russia.
(last modified 2024-09-27T03:15:38+00:00 )
Sep 27, 2024 03:15 UTC
  • Ulaya ni muhali kuafikiana kuhusu vita dhidi ya Russia

Wakati Rais wa Russia ameonya kuhusu madhara yasiyotabirika ya kutumiwa silaha za nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo, imedhihirika wazi kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuchukua uamuzi wa pamoja wa kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za Magharibi kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Russia.

Shirika la habari la Interfax limeripoti kuwa, maafisa wa Brussels wametangaza kwamba Umoja wa Ulaya hautochukua uamuzi wa pamoja wa kutumiwa silaha za Magharibi inazopewa Ukraine kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Russia.

Wakati huo huo, Rais Vladimir Putin wa Russia ameonya waziwazi kuhusu madhara yasiyotabirika ya kutumiwa silaha za Magharibi dhidi ya nchi yake. Alitoa onyo hilo juzi Jumatano akisema wazi kwamba, msimamo wake wa kutotumia silaha za nyuklia unategemea ukubwa wa vitisho na hatari inayoikabili nchi yake.

Naye Peter Stano, msemaji wa sera za kigeni ya Umoja wa Ulaya, alisema Jumatano usiku baada ya onyo la Rais wa Russia kwamba uamuzi wa kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za Magharibi katika mashambulizi ya ndani kabisa ya ardhi ya Russia uko mikononi mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, na kwamba Kamisheni ya Ulaya haiwezi kuruhusu kufanyika mashambulizi kama hayo.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba, bila ya shaka, Ukraine ina haki isiyopingika ya kushambulia maeneo ya kijeshi ndani ya ardhi ya Russia, lakini uamuzi wa kutumia silaha ilizopewa na Umoja wa Ulaya uko mikononi mwa nchi wanachama wa umoja huo na si rahisi kupata kauli ya pamoja ya wanachama hao kuhusu suala hilo.