EU yamtetea katibu Mkuu wa UN, yaponda madai ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i117056-eu_yamtetea_katibu_mkuu_wa_un_yaponda_madai_ya_israel
Mkuu wa Siasa za Kigeni za Umoja wa Ulaya ameeleza masikitiko yake kutokana na tuhuma zilizotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusema kuwa Umoja wa Ulaya unaunga mkono juhudi za Antonio Guterres za kuimarisha amani.
(last modified 2024-10-03T05:44:05+00:00 )
Oct 03, 2024 05:44 UTC
  • Josep Borrell
    Josep Borrell

Mkuu wa Siasa za Kigeni za Umoja wa Ulaya ameeleza masikitiko yake kutokana na tuhuma zilizotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusema kuwa Umoja wa Ulaya unaunga mkono juhudi za Antonio Guterres za kuimarisha amani.

Ni baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kumtaja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuwa ni mtu asiyetakikana eti kwa sababu ya kunyamazia kimya operesheni ya makombora ya Iran ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel, na kumpiga marufuku kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Uamuzi huo wa Israel umepingwa vikali na shakhsia wengi duniani ambao wameutaja kuwa ni kinyume na juhudi za kuimarisha amani katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Josep Borrell, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ameeleza masikitiko yake kuhusu uamuzi wa Israel wa kumpiga marufuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusema: Umoja wa Ulaya unamuunga mkono Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na juhudi zake za kupatikana amani katika migogoro yote hasa Mashariki ya Kati.

Borrell ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unaona kuwa mashambulizi yasiyo ya haki dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na pia mauaji ya idadi kubwa ya wafanyakazi wa shirika hilo la kimataifa katika mashambulizi ya utawala unaofanya mauaji ya kimbari wa Israel hayawezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. 

Taarifa iliyotolewa hapo awali na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu inasema: Baada ya muda wa kujizuia mbele ya ukiukwaji wa mamlaka ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia mauaji yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Mujahid Ismail Haniyeh, na kwa mujibu wa haki ya nchi ya kujilinda chini ya Hati ya Umoja wa Mataifa, na kutokana na kushadidi maovu ya utawala huo ghasibu ukiungaji mkono na Marekani katika mauaji ya halaiki ya wananchi wa Lebanon na Gaza na kumua shahidi Mujahid mkubwa, kiongozi wa Mhimili wa Muqawama na Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah, na kuuawa shahidi Kamanda na mshauri wa ngazi ya juu wa IRGC huko Lebanon, Meja Jenerali Abbas Nilforoushan, Kikosi cha Anga cha IRGC kumepiga maeneo muhimu ya kijeshi na kiusalama katika moyo wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel).

Taarifa iliyotolewa juzi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilisema: Iwapo utawala wa Kizayuni utachukua hatua za kijeshi baada ya operesheni hiyo ambayo imefanyika kwa mujibu wa haki za kisheria za nchi na sheria za kimataifa, itakabiliwa kwa mashambulizi shadidi na yenye uharibifu mkubwa zaidi.