Reuters: BRICS kujadili mpango mpya wa kimataifa wa mabadilishano ya fedha
Russia itawasilisha pendekezo lake la mfumo mpya wa fedha wa kimataifa kwa mataifa mengine wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya BRICS katika mkutano wa kilele wa kundi hilo utakaofanyika wiki ijayo nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Reuters likinukuu waraka uliosambazwa na Moscow kwa waandishi wa habari kabla ya mkutano huo.
Reuters imeeleza kuwa, mfumo huo wa fedha unaaminika kuwa hautaweza kuathiriwa na vikwazo vya Magharibi na unaweza kukomesha ukiritimba wa sarafu ya dola ya Marekani katika mabadilishano ya kimataifa na miamala ya kifedha.
Kulingana na ripoti hiyo, mfumo huo utaruhusu na kuwezesha kufanyika mabadilishano ya fedha kwa urahisi na kwa usalama bila ya hitaji la kila mahali la shughuli za dola. Aidha utategemea mtandao wa benki za biashara zilizounganishwa kupitia benki kuu za nchi wanachama wa BRICS.
Pendekezo hilo pia linasemekana kuhusisha kuundwa kwa jukwaa liitwalo ‘BRICS ya Wazi’ ili kusuluhisha biashara ya dhamana.
Kwa mujibu wa Reuters, hati hiyo ya pendekezo la Russia inazishutumu pia taasisi za fedha za kimataifa zilizopo, ikiwa ni pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa, kwa kutumikia maslahi ya Marekani na washirika wake.
Moscow haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti hiyo ya Reuters na haijaweka hadharani hati yoyote kama ile iliyotajwa ndani yake.
Hata hivyo wiki iliyopita, Waziri wa Fedha wa Russia Anton Siluanov aliwasilisha pendekezo la mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa kwa mawaziri wengine wa fedha na wakuu wa benki kuu za mataifa wa nchi wanachama wa BRICS.../