Wasiwasi wa Ulaya kuhusu kurejea Trump White House
Matokeo ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani yamegubika hali ya siasa, uchumi na usalama wa Ulaya.
Siku moja baada ya kutangazwa ushindi wa Trump katika uchaguzi huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwa bara hilo linapasa kutangaza uhuru wake wa kiusalama kutoka kwa Marekani na kutetea maslahi yake mkabala wa maslahi ya wapinzani wake wa kijiografia.
Rais wa Ufaransa ameeleza kuwa: 'Ulaya haipasi kuipatia Marekani usalama wake milele na inapasa hivi sasa kuchukua hatua ili isidhoofishwe kijiografia. Watu wa Ulaya wanapasa kuchukua hatua kubwa kutetea maslahi yao dhidi ya Marekani na China.'
Nchi za Ulaya hazina rekodi nzuri kuhusu urais wa miaka minne wa Trump kuanzia mwaka 2017 hadi 2021. Umoja wa Ulaya hasa mhimili wa Ujerumani na Ufaransa nchi mbili ambazo ni nguvu kuu ya umoja huo zilikuwa na uhusiano wenye changamoto kati yazo na Marekani katika miaka hiyo minne. Trump alipinga uhusiano mkubwa kati ya washirika wa pande zote mbili za Bahari ya Atlantiki katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiusalama, kuanzia masuala ya mazingira hadi ushirikiano wa kijeshi na kiusalama katika mkataba wa NATO.
Ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa 2020 ulikuwa habari njema kwa ajili ya kurejea uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya Ulaya na Marekani kabla ya Trump kuwa Rais wa Marekani. Hata hivyo, kurejea Trump huko White House ni jinamizi kwa serikali za Ulaya. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Ulaya pia uko katika hali tete ambapo Umoja huo unalegalega katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Tofauti na miaka minane iliyopita, Umoja wa Ulaya unakabiliwa na migogoro mikubwa ya ndani katika ngazi ya Ulaya na kimataifa. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholtz na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika mkutano wa viongozi wa nchi za Ulaya wamejaribu kuonyesha kuwa wapo tayari kukabiliana na kurejea Trump katika Ikulu ya White House. Macron na Scholtz wamempongeza Trump kwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Jumanne iliyopita hata hivyo wametilia mkazo kuhusu changamoto zinazosababishwa na sera ya biashara ya Trump, ambayo inakuzwa kwa kauli mbiu ya "Marekani Kwanza".
Scholtz amewaambia waandishi wa habari kwamba Umoja wa Ulaya unapasa kuimarisha kwa nguvu safu zake na kuchukua hatua kwa pamoja. Ameongeza kuwa, yeye na Macron wanawasiliana kwa karibu na viongozi wengine wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya. Macron pia amesema katika mahojiano ya televisheni kuwa Berlin na Paris zitafanya kazi kwa ajili ya Ulaya yenye umoja na imara zaidi katika mazingira mapya.
Scholtz na Macron wanazungumzia suala la kukabiliana nna changamoto za kurejea Trump huko White House katika hali ambayo viongozi hao wawili ndani ya nchi zao wenyewe wako katika hali ngumu. Serikali ya muungano ya Ujerumani imeanguka siku moja baada ya kuchaguliwa Rais wa Marekani. Mawaziri wanne wa chama cha Wademocrat cha Uhuru wamejitoa katika serikali ya Ujerumani wakilalamikia mpango wa bajeti ya mwaka ujao ya Kansela wa nchi hiyo Olaf Scholtz. Kwa utaratibu huo, kwa mara ya kwanza baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani itaendesha uchaguzi wa mapema wa bunge mwishoni mwa mwezi machi mwakani. Wakati huo huo, chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo mikali cha Alternative for Germany kimepata ushindi mkubwa katika chaguzi tatu za majimbo. Ushindi huu wa sasa wa vyama vya mrengo wa kulia vyenye siasa kali nchini Ujerumani unagubika siasa za nchi hiyo. Uwepo madarakani wa vyama hivyo vya siasa kali ni changamoto kwa mradi wa ushirikiano wa Ulaya. Hasa ikizingatiwa kuwa vyama hivyo vya mrengo wa kulia huwa vinashirikiana na kwenda sambamba na Donald Trump.
Emmanuel Macron pia anakabiliwa na hali ngumu huko Ufaransa. Macron alishindwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya na katika uchaguzi wa mapema wa bunge la nchi hiyo. Katika upande wa Ulaya, vita vya Ukraine vimevuruga milinganyo yote ya kisiasa na kiusalama barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Ukraine imekuwa eneo kwa ajili ya vita vya niaba vya Nato na Russia huku Marekani ikiipatia Ukraine asilimia sabini ya misaada ya kifedha na kijeshi. Trump alitangaza kabla ya uchaguzi kuwa atahitimisha vita vya Ukraine katika muda wa miezi miwili iliyosalia hadi kufanyika hafa ya kuapishwa Rais wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo jeshi la Ukraine halitarajii kuishinda Russia katika vita hivyo. Kinyume chake, Russia inaendelea kusonga mbele huko Ukraine. Kwa hiyo, njia pekee aliyonayo Trump ni kutambua rasmi kusonga mbele kwa Russia na kufikia suluhu na Putin.
Katika uga wa kiuchumi, kauli mbiu ya Trump ya "Marekani Kwanza" ni hatari kwa uchumi wa Ulaya. Ujerumani iko kwenye mdororo wa uchumi kwa mwaka wa pili mtawalia sasa. Nakisi ya bajeti na ukubwa wa madeni yanayoisibu Ufaransa pia vimepindukia viashiria vya Umoja wa Ulaya. Wakati huo huo, mpango wa Trump wa kuongezesha ushuru kwa bidhaa kutoka nje utazidisha gharama ka mauzo ya nje na kushadidisha mfumuko wa bei barani Ulaya.
Umoja wa Ulaya katika miaka minne ijayo utakuwa na uhusiano wenye changmoto nyingi kati yake na Marekani chini ya uongozi wa Trump kutokana na kutokuwa na sera ya pamoja kuhusu mambo ya nje, usalama, matatizo ya kiuchumi na hatari ya kuongezeka wanaiasia wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia barani humo.