Lavrov akosoa jitihada za Magharibi za kueneza chuki dhidi ya Russia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amekosoa vikali njama za nchi za Magharibi za kueneza chuki dhidi ya nchi hiyo.
Sergei Lavrov amekosoa njama za Magharibi za kuzichochea nchi nyingine kubadili mtazamo wao kuhusu Russia na kusema: Nchi za Magharibi zinattumia vitisho ili kuzuia kuundwa ulimwengu wa kambi kadhaa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza hayo katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Viongozi wa Ngazi ya Juu wa Russia na Nchi za Afrika katika mji wa Sochi huko Russia.
Lavrov ameashiria namna nchi za Magharibi zisivyotaka kupoteza nafasi yake ya juu kimataifa na akasema: Njia ambazo Wamagharibi wanazitumia katika uhusiano na akthari ya nchi za dunia hazina tofauti na mbinu za kikoloni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa, Russia na Afrika zimewasilisha mapendekezo ya kuboresha uhusiano kati yao na kuhakikisha mabadilishano baina yao yanafanyika bila ya vitisho. Amesema: "Moscow hadi sasa haijawahi kuzikoloni nchi za Kiafrika kinyume na nchi za Magharibi."
Rais Vladmir Putin wa Russia jana alituma ujumbe katika mkutano wa Sochi akisisitiza kwamba: Moscow itaendelea kuziunga mkono kikamilifu nchi za Afrika katika nyanja zote ikiwemo vita dhidi ya ugaidi na kuzisaidia pia kupambana na mgogoro wa chakula.
Russia na nchi za Afrika zilifanya mikutano ya wakuu wa nchi katika miaka ya 2019 na 2023.