Lavrov: Russia itatumia 'njia yoyote' kuhakikisha haishindwi katika vita vya Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119800-lavrov_russia_itatumia_'njia_yoyote'_kuhakikisha_haishindwi_katika_vita_vya_ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, kutumiwa hivi majuzi na jeshi la nchi yake kombora la hypersonic katika vita vya Ukraine kumelenga kuzielewesha nchi za Magharibi kwamba Moscow iko tayari kutumia "njia yoyote" ili kuzuia kushindwa katika vita hivyo.
(last modified 2024-12-07T02:24:28+00:00 )
Dec 07, 2024 02:24 UTC
  • Sergey Lavrov
    Sergey Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, kutumiwa hivi majuzi na jeshi la nchi yake kombora la hypersonic katika vita vya Ukraine kumelenga kuzielewesha nchi za Magharibi kwamba Moscow iko tayari kutumia "njia yoyote" ili kuzuia kushindwa katika vita hivyo.

Lavrov ameyasema hayo katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Marekani Tucker Carlson na akabainisha kwamba nchi za Magharibi zinapigania kuzatiti ukiritimba wao duniani kote, katika nchi yoyote, eneo lolote na katika bara lolote, wakati Moscow inapigania maslahi yake halali ya kiusalama. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: "tunatuma salamu za ishara na tunatumai kuwa zile za mwisho tulizotuma wiki chache zilizopita, ambazo ni za ishara iliyoambatana na mfumo mpya wa silaha unaoitwa Oreshnik zimezingatiwa kwa uzito".

Katika mahojiano hayo, Lavrov ameeleza pia kwamba japokuwa Russia haitaki kuzidisha mivutano na inataka kuepusha hali ya kutoelewana na Washington na waitifaki wake, lakini ameonya kwa kusema: "tutatuma salamu za ziada ikiwa hawatafikia hitimisho muhimu".

Kuhusiana na chanzo cha vita vya Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: “sisi hatukuanzisha vita hivi. Tumekuwa kwa miaka na miaka na miaka tukitoa indhari kwamba kuisukuma NATO karibu zaidi na mipaka yetu kutasababisha tatizo".

Katika mahojiano hayo ya dakika 80 na Carlson, Lavrov amebainisha pia kuwa nchi za Magharibi zinapaswa kuachana na dhana yoyote ile ya kuchukulia kwamba Russia haina "mistari myekundu".../