Mazungumzo yaliyogubikwa na mvutano mkubwa kati ya Trump na Zelensky
Viongozi wenye mielekeo ya Kimagharibi wa Ukraine waliipa mgongo Russia baada ya matukio ya mwaka 2014 na kuingia madarakani serikali kibaraka kwa Magharibi huko Ukraine kwa himaya na msaada wa pande zote wa nchi za magharibi hususan Marekani na Ulaya; na walitaka nchi hiyo kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na Umoja wa Ulaya (EU) na kukata uhusiano na Russia.
Hatimaye hatua hizi zilipelekea kujiri vita vya umwagaji damu na uharibifu mkubwa tangu mwishoni mwa Februari 2022 hadi sasa. Sasa, matumaini na ndoto zote za Ukraine za kujiunga na kambi ya Magharibi zimesambaratishwa na mazungumzo yaliyogubikwa na mvutano kati ya Trump na Zelensky, Marais wa Marekani na Ukraine mjini Washington hiyo jana Ijumaa.
Mazungumzo ya kihistoria kati ya Rais wa Marekani Donald Trump, Makamu wake D.J. Vance pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky jana Ijumaa, Februari 28, katika Ikulu ya White House yaligeuka na kuwa mabishano makali kati ya pande mbili mbele ya kamera za vyombo vya habari vya dunia, ambapo Trump na makamu wake walimdhalilisha wazi wazi mgeni wao, huku Trump akimfokea Zelensky mara kwa mara mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais. Itakumbukwa kuwa Zelensky alielekea Washington kwa lengo la kutia saini mkataba wa kukabidhi mgodi wa madini nadra wa Ukraine kwa Washington.
Hali ilizidi kuwa tete baada ya Rais wa Ukraine kujibu kauli za Makamu wa Rais wa Marekani J.D Vance aliyekuwepo kwenye mazungumzo hayo aliposema njia ya amani ni kupitia diplomasia na Russia. Vance alisema: "Ukraine inakabiliwa na matatizo makubwa katika vita." Akimhutubu Zelensky, D.J. Vance alisema: "Unapasa kumshukuru Rais kwa jitihada zake za kumaliza mzozo huo." Zelensky alisema kuwa Marekani pia inakabiliana na matatizo yake yenyewe, na kwamba amesikia maneno haya kutoka kwa Putin, lakini Trump alikatisha maneno yake mara moja. Trump alimfokea Zelensky na kumwambia: "Wewe haupo katika nafasi nzuri na huna turufu mkononi mwako. Unacheza na maisha ya mamilioni ya watu. Unacheza kamari na Vita vya Tatu vya Dunia na unachofanya ni dharau sana kwa Marekani. Unapasa kushukuru."
Rais wa Marekani aliyataja matamshi ya Zelensky kuwa "ya kukosa heshima" kisha akamtishia kwa kusema: "Kama si silaha zetu, vita hivi vingeisha haraka sana. Inabidi ukubaliane au hatutaingilia kati tena. Huna uwezo wa kutosha, huwezi kutuambia kama unataka kusitisha mapigano au la."

Kufuatia mabishano makali ya maneno kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, makamu wake D.J Vance na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mbele ya vyombo mbalimbali vya habari vya dunia, Trump alimfukuza Zelensky na ujumbe wa Ukraine katika Ikulu ya White House mjini Washington. Waukraine wamelalamikia kitendo hicho na kuomba mazungumzo yaendelee. Hata hivyo ombi hilo limekataliwa. Zelensky aliondoka White House muda mfupi baada ya ombi hilo.
Wakati huo huo ikulu ya White House ilimtaka Volodymyr Zelensky kumuomba radhi Donald Trump, lakini alikataa kufanya hivyo katika mahojiano na Fox News, chombo cha habari chenye uhusiano na chama cha Republican, na akamshukuru tu Trump na wananchi wa Marekani.
Mazungumzo hayo yaliyojaa mabishano yamepokewa kwa hisia tofauti ndani ya Marekani na kimataifa. Lindsey Graham, seneta wa chama cha Republican nchini Marekani amemkosoa Rais wa Ukraine akisema: Zelensky anapasa kuomba radhi, la sivyo Ukraine itume mtu mwingine au ibebe dhima na hatua hiyo. Katika upande wa pili, Ssneta wa chama cha Democratic, Jack Reed amemkosoa Trump na serikali yake na kusema: Trump na makamu wake D. Vance wanaieleza dunia kwamba Marekani si nchi ya kuaminiwa.
Viongozi wa Ulaya wametangaza uungaji mkono wao kwa Ukraine baada ya mazungumzo hayo ya mvutano na mabishano makubwa kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine. Kinyume chake, Dmitry Medvedev Rais wa zamani wa Russia na Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la nchi hiyo amesema: Kofi ambalo Trump na D. Vance wamemzaba Zelensky linafaa lakini halitoshi.

Tunaweza kusema kuwa, kwa kuzingatia misimamo ya huko nyuma ya Trump, iwe wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais mwaka jana au baada yake na wakati alipoingia White House katika duru ya pili ya urais wake, ilitabiriwa kuwa anataka kumtwisha Zelensky matakwa yake, na akubali hali iliyopo sasa na aikabidhi Russia ardhi iliyovamiwa ya Ukraine, yaani akabidhi karibu asilimia 20 ya ardhi ya nchi hiyo, na pia akubali kusaini mkataba uliopendekezwa na Trump wa kuipa Marekani mgodi wa madini adimu wenye thamani ya dola zisizopungua bilioni 500 mkabala wa kile kinachodaiwa na Washington kuwa kuidhaminia Ukraine usalama wake. Lakini jambo ambalo halikutarajiwa katika mkutano huo ni kusimama ngangari Zelensky mbele ya Trump kwa upande mmoja, na kudhihirika hulka ya kiburi na kujiona bora Marekani kufuatia matamshi ya fedheha na ya udhalilishaji ya Trump na makamu wake, Vance mkabala wa Zelensky Zelensky, tena mbele ya kamera za vyombo vya habari vya Marekani na kimataifa. Kwa mwenendo huu, Trump ameonyesha kuwa kitendo cha Marekani cha kujiona bora na kuwa juu ya nchi nyingine ni hulka ya kawaida ya viongozi wa nchi hiyo ambao hawaheshimu nchi nyingine wala viongozi wa nchi hizo.
Katika upande mwingine, uzoefu wa Ukraine na kufuata kwake kibubusa ahadi za nchi za Magharibi hasa Marekani, na hatua yake ya kujitumbukiza katika vita na Russia huku ikisisitiza kupatiwa uanachama ndani ya NATO licha ya tahadhari za Russia, jambo ambalo mwishowe lilipelekea kuanza vita kati ya Russia na Ukraine, unaonyesha kuwa kuitegemea Marekani na misaada ya nchi hiyo hatimaye kunaweza kusababisha athari mbaya na za uharibifu kwa nchi mbalimbali. Hasa ikizingatiwa kuwa, Trump kwa kudai kuwa ni lazima Marekani imiliki madini ya thamani kubwa ya Ukraine na kwamba Kyiv inapasa kulipa dola zisizopungua bilioni 500 mkabala wa misaada ya eti thamani ya dola bilioni 350 ambayo Washington inadai kuipatia Kyiv inaonyesha kuwa Marekani, licha ya nara na shaari kubwa inazotoa kama nara za kupigania uhuru, uadilifu na demokrasia kwa ajili ya nchi mbalimbali, lakini kidhahiri nchi hiyo inafuatilia maslahi yake binafsi hususan maslahi ya kiuchumi.
Kwa utaratibu huu, tunapasa kusema kuwa mazungumzo ya mvutano mkubwa kati ya Trump na Zelensky ni sawa na kufikia ukomo njozi na ndoto ya kupata amani, uhuru, demokrasia na ustawi wa kiuchumi kupitia njia ya kuzitegemea nchi za Magharibi hususan Marekani.