UN: Tuna wasiwasi kuhusu mwelekeo wa White House
Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk ameelezea wasiwasi wake kuhusu mabadiliko ya mwelekeo yanayofanyika nchini Marekani katika uwanja wa ndani na kimataifa.
Bila kumtaja moja kwa moja kwa jina Rais Donald Trump wa Marekani, Volker Turk amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu mabadiliko ya mwelekeo yanayofanyika Marekani kuhusu masuala ya ndani na nje ya nchi.
Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa sera zilizowekwa kwa lengo la kuwalinda watu dhidi ya ubaguzi wa rangi sasa zinatambuliwa kuwa "za kibaguzi."
Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba matamshi hayo ya Volker Turk katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva ndiyo makali zaidi kuwahi kutolewa hadi sasa kuhusu athari mbaya za sera za serikali mpya ya Marekani.
Mbali na kutia saini amri ya kujiondoa nchi yake katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Donald Trump pia ametia saini amri ya utendaji ya kupiga marufuku ufadhili wa Marekati kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).