Uturuki yawapiga kalamu nyekundu wanajeshi 1,400
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12349-uturuki_yawapiga_kalamu_nyekundu_wanajeshi_1_400
Uturuki imewapiga kalamu nyekundu takriban maafisa 1,400 wa jeshi la nchi hiyo, wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na Fethullah Gulen, raia wa nchi hiyo anayeishi Marekani anayetuhumiwa kupanga mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2016 11:49 UTC
  • Uturuki yawapiga kalamu nyekundu wanajeshi 1,400

Uturuki imewapiga kalamu nyekundu takriban maafisa 1,400 wa jeshi la nchi hiyo, wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na Fethullah Gulen, raia wa nchi hiyo anayeishi Marekani anayetuhumiwa kupanga mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli.

Habari hizo zinajiri muda mfupi baada ya Rais Recep Teyyip Erdogan wa nchi hiyo kutangaza kuwa anapania kufanya mabadiliko katika jeshi la nchi hiyo ikiwemo kufunga taasisi zote za kutoa mafunzo ya jeshi na kufungua chuo kikuu kimoja kwa ajili ya kozi hiyo.

Rais Recep Teyyip Erdogan wa Uturuki akikagua gwaride

Habari zinasema kuwa, Rais Erdogan anapanga kuwasilisha muswada bungeni ambao iwapo utapasishwa na kuwa sheria, Shirika la Taifa la Ujasusi sasa litakuwa chini ya Ofisi ya Rais moja kwa moja sanjari na kuwataka makamanda wakuu wa vikosi vya ardhini, baharini na angani kuripoti moja kwa moja kwa Waziri wa Ulinzi Fikri Isik.

Hii ni katika hali ambayo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza masikitiko yake juu ya kukithiri ukandamizaji, kamata kamata na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Uturuki, baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofeli.

Maandamano ya kulaani jaribio la mapinduzi ya kijeshi

Katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ambalo lilitekelezwa na baadhi ya askari wa jeshi la Uturuki, karibu watu 300 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa mujibu wa duru za habari nchini Uturuki karibu watu 50 elfu kati ya maafisa wa serikali wametiwa mbaroni na kusimamishwa kazi kufuatia tukio hilo.