Russia yaitaka Ulaya iache vitisho dhidi ya Iran
(last modified Thu, 06 Mar 2025 02:29:00 GMT )
Mar 06, 2025 02:29 UTC
  • Russia yaitaka Ulaya iache vitisho dhidi ya Iran

Russia imekosoa vikali vitisho vya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani vya kuamilisha mchakato wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran na kutaja msimamo huo kuwa wa "kutowajibika" na "ulio kinyume cha sheria".

Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Mwakilishi Mkuu wa Russia katika Mashirika ya Kimataifa huko Vienna, Mikhail Ulyanov amesema kuwa, baada ya kukiuka majukumu yao chini ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na makubaliano ya JCPOA, nchi hizo tatu za Ulaya zinapania kuiadhibu Iran kwa tuhuma za kutoheshimu makubaliano ambayo wao wenyewe waliyavunja mnamo Agosti 2022.

"Tunatiwa wasi wasi na vitisho vya Uingereza, Ujerumani na Ufaransa vya kutumia mchakato wa 'snapback'. Tunayatazama maneno kama haya kuwa sio tu ya kutowajibika, lakini pia ni kinyume cha sheria," amesisitiza Ulyanov.

Mchakato wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran chini ya makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 unaojulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), unaruhusu pande zote katika mapatano hayo kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran iwapo itakiuka makubaliano hayo.

Trump alipoiondoa US katika makuabaliano ya JCPOA 2018

Hata hivyo, mwaka 2018, Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano ya JCPOA na kutekeleza sera ya "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, huku pande nyingine za mapatano hayo - Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia na China - zikishindwa kulinda maslahi ya Iran chini ya makubaliano hayo.

Iran ilisubiri mwaka mzima baada ya Marekani kujiondoa kwenye JCPOA, huku madola matatu ya Ulaya yakiahidi kupunguza athari za vikwazo vya Marekani; lakini kutokana na jitihada hizo kushindwa, hatimaye Tehran ilianza kupunguza majukumu yake kwa mujibu wa vipengee vya mapatano hayo ya kimataifa.