Trump na kukandamizwa uhuru wa kusema huko Marekani
(last modified Sat, 08 Mar 2025 04:23:46 GMT )
Mar 08, 2025 04:23 UTC
  • Trump na kukandamizwa uhuru wa kusema huko Marekani

Gazeti la Marekani la Washington Post limeandika makala likiashiria amri za utendaji zilizotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, tangu aingie madarakani na kusema: Wakosoaji wanamtuhumu kuwa anakandamiza sana uhuru wa kujieleza na kukiuka Katiba ya Marekani.

Wanasema kwamba Trump anajaribu kuondoa “WOKE” (itikadi inayomaanisha kuwa macho kuhusu masuala ya haki ya kijamii na uadilifu wa kimbari), ambako kunakinzana na Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani.

Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, yaliyoidhinishwa mwaka wa 1791, yanakataza serikali kutunge sheria zinazothabitisha dini fulani kama dini rasmi, kupinga uhuru wa itikadi ya dini, au kukandamiza uhuru wa kusema na kujieleza, haki ya kukusanyika kwa amani, au haki ya kufungua mashtaka ili kupata fidia ya hasara kutoka kwa serikali.

Trump na mshirika wake, bilionea Elon Musk, wamejidhihirisha kama watiifu katika suala la uhuru wa kujieleza na wanajaribu kuirejesha Marekani katika mwelekeo huo huo baada ya miaka ya waliberali kujaribu kunyamazisha sauti za kihafidhina.

Trump ameibuka kuwa rais wa nchi ya demokrasia ya kiliberali huku akiwa na mawazo na mwelekeo wa kimabavu na kifashisti. Mfano wa hilo ni kufurahishwa kwake na picha yake kwele jalada la gazeti la Time, lililomwita mfalme. Tangu Trump aingie madarakani, Januari 20, wakosoaji wanasema ameanzisha mashambulizi mengi dhidi ya uhuru wa kujieleza; ikiwa ni pamoja na juhudi zake za kufutilia mbali sera ya Diversity, Equity, and Inclusion (DEI), ambayo lengo na kauli mbiu yake ni kuwapa kazi na ajira watu wa mbari tofauti au ulemavu. Ikulu ya White House pia imepiga marufuku Associated Press kuingia ndani ya jengo hilo na kuripoti matukio na habari kwa sababu ya kuendelea kutumia jina la Ghuba ya Mexico badala ya Ghuba ya Marekani.

Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa urais wake, Trump alitoa agizo la kubadilishwa jina la Ghuba ya Mexico na kuwa Ghuba ya Marekani. 

Gazeti la Washington Post limeyataja mashambulizi ya Trump na timu yake dhidi ya uhuru wa kujieleza kuwa ni aina fulani ya kutupilia mbali itikadi ya "WOKE" (ufahamu wa haki za kijamii na umakini dhidi ya ubaguzi wa rangi) ambayo inaionyesha Marekani kama nchi ya ubaguzi wa rangi na wa kijinsia.

Katika hatua yake ya hivi karibuni dhidi ya uhuru wa kujieleza, Rais wa Marekani ametishia kukata bajeti ya Shirikisho kwa vyuo vikuu vinavyofanya maandamano ya kupinga Uzayuni na kuwaunga mkono Wapalestina. Trump alitangaza kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii la Truth Jumanne iliyopita kwamba ufadhili wote wa Shirikisho kwa vyuo vikuu na shule zinazoruhusu maandamano "haramu" utasitishwa, na kwamba "wafanya ghasia" watafungwa au kurudishwa katika nchi walikotoka.

Ukweli ni kwamba, kilichoshuhudiwa  na ulimwengu baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani wa Novemba 2024 haukuwa ushindi wa mgombea wa chama kimoja na kushindwa mgombea wa chama kingine, kwa mujibu wa utamaduni wa jadi wa uchaguzi wa Marekani, bali ni kuibuka mwelekeo wenye msimamo mkali unaolenga kuvuruga sheria zote zilizowekwa tangu kuanzishwa kwa Marekani, kwa msingi wa fikra za wanafalsafa kama John Locke na wanafalsafa wengine wa kiliberali. Marekani ya Trump sasa inajitenga kabisa na sheria zote hizo, kanuni na maadili ya uliberali ambayo wanafalsafa kama Francis Fukuyama alidai katika kitabu chake maarufu, "The End of History and the First Man," kuwa ni ushindi mutlaki wa demokrasia ya kiliberali. Sasa Fukuyama na wanafalsafa wenzake wanaomboleza kifo cha uliberali huko Marekani.

Sauti inayosikika kutoka Marekani hii leo, pamoja na misimamo na mienendo ya Trump na watu wengine wenye fikra kama zake katika serikali yake, ni mabadiliko ya kimsingi katika mwelekeo wa sera ya Marekani ambayo yamewashangaza na kuwaacha bumbuazi hata washirika wa karibu wa Marekani barani Ulaya, Asia, Mashariki ya Kati na kadhalika. Sasa sauti ya ufashisti inasikika kutoka kwa Trump na Makamu wake, J.D. Vance. Kwa kuzingatia hotuba za hivi majuzi za Vance huko Ulaya, sasa anatambulika katika duru za kisiasa za Ulaya kama "Mussolini wa pili," na vyama vyenye siasa kali za mrengo wa kulia barani humo vinatazamia uungwaji mkono wa kisiasa na kifedha wa Trump na timu yake, pamoja na Elon Musk, ili kupata nguvu ya kisiasa na kunyakua madaraka.

Athari mbaya ya kuibuka tena Donald Trump katika uga wa siasa wa Marekani na matokeo yake kwa nchi hiyo, Ulaya, na sehemu nyingine za dunia inaweza kueleweka wakati kuchunguzwa kwa kina falsafa na sababu ya kuwepo kwa watu kama Elon Musk, mwenye utajiri wa dola bilioni 420, na makumi ya matajiri wengine wabwa katika utawala wa Trump, ambao utajiri wao unazidi bajeti ya kila mwaka ya nchi 70.

Elon Mask na Trump katika White House

Inaonekana kwamba moja kati ya malengo ya Trump ni kuandaa nafasi na uwanja unaohitajika kwa ajili ya shughuli za matajiri hao wakubwa kupata faida zaidi na kukandamiza fikra au harakati yoyote inayopinga mawazo, mbinu na sera za utawala wa Trump.