Maafisa wa US yumkini wakapelekwa ICC kwa kuzuia haki
Afisa wa zamani wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Craig Mokhiber ameonya kuwa, maafisa wa Marekani wanaoishambulia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC katika kuitetea Israel wanazuia haki na sheria, na kusisitiza kwamba wanaweza kushtakiwa katika siku zijazo.
Mokhiber ameiambia Al Jazeera kwamba, tawala zote mbili za (Marekani za) Joe Biden na Donald Trump zimeiruhusu Israel kukanyaga haki za wakazi wa Gaza na Palestina kwa ujumla.
Ameeleza kuwa, utawala wa Trump umefikia hatua ya kuwakamata watu nchini Marekani "kwa kuukosoa utawala dhalimu wa Israel kwa sababu unafanya mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi."
Amesema kukamatwa kwa mwanaharakati na msomi wa Kipalestina, Mahmoud Khalil ni ishara ya shambulio pana zaidi dhidi ya haki za binadamu.
Mokhiber ameongeza kwamba, matukio haya yanapaswa kuonekana katika muktadha wa hujuma ya Marekani dhidi ya taasisi za kimataifa za kulinda na kutetea haki za binadamu.
Afisa huyo wa zamani wa UN amebainisha kuwa, "Utawala wa Trump tayari umeishambulia ICC, kitendo ambacho ni uhalifu katika sheria za kimataifa, sawa na kuzuia haki."
Mokhiber ameongeza kuwa, mahakama ya ICC yenyewe ina mamlaka na uwezo wa kuwashtaki maafisa wa Marekani na Israel kwa kuzuia haki na kuwa kizingiti katika mkondo wa utekeleza wa sheria.