Russia nayo yaionya Washington kuhusu shambulio lolote dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i124644-russia_nayo_yaionya_washington_kuhusu_shambulio_lolote_dhidi_ya_vituo_vya_nyuklia_vya_iran
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameonya kwamba shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran linaweza kuwa na madhara makubwa kwa eneo zima la Mashariki ya Kati.
(last modified 2025-04-02T02:30:09+00:00 )
Apr 02, 2025 02:30 UTC
  • Sergei Ryabkov
    Sergei Ryabkov

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameonya kwamba shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran linaweza kuwa na madhara makubwa kwa eneo zima la Mashariki ya Kati.

Sergei Ryabkov ameonya kuhusu hatua zozote za kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, akisisitiza kwamba mashambulizi hayo yatakuwa na matokeo hatari kwa kanda nzima ya Magharibi mwa Asia.

Ryabkov amesema kuwa kulenga na kulipua miundombinu ya nyuklia ya Iran kunaweza kuhatarisha usalama wa kikanda na kuwa na athari mbaya.

Hapo awali pia maafisa wa serikali ya Russia walikuwa wameeleza wasiwasi wao kuhusu vitendo vyovyote vya uchochezi ambavyo vitatishia usalama na amani Asia Magharibi. Kauli hii imetolewa baada ya Marekani kutaka kuzua hali ya wasiwasi katika eneo hilo kwa kudai kuwa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran sio ya amani.

Hii ni licha ya kuwa shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa zikifanyika kwa uwazi na kwa malengo ya amani na zinafanyika ndani ya fremu ya majukumu ya Iran chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji silaha la Nyuklia. Kinyume chake, Marekani ndiyo nchi pekee ambayo imewahi kutumia silaha za nyuklia na kufanya uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu kwa kuua maelfu ya watu nchini Japan kwa kutumia silaha za nyuklia.

Wakati huo huo, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ameionya Marekani kuhusu uwezekano wa kushambulia ardhi ya Iran na kusema, wanajeshi wa Marekani katika eneo hili wapo katika "nyumba ya vioo" na wanapaswa kuepuka "kuwarushia wengine mawe."