Ripoti: Putin analenga 'adui mpya wa Kimagharibi': Waabudu Shetani
Rais wa Russia, Vladimir Putin na washirika wake wamevitaja vita vya Ukraine kuwa vita dhidi ya waabudu mashetani, na vilevile dhidi ya sera zinazounga mkono vitendo vya maingiliano ya kingono baina ya watu wenye jinsia moja (LGBTQ) za Magharibi, ambazo wanaona kuwa zinadhoofisha maadili ya jadi ya Kikristo.
Katika ripoti yake kuhusu suala hilo, gazeti la The Times limeutambua msimamo huo kuwa ni mabadiliko makubwa kutoka enzi ya Muungano wa Sovieti, wakati kutokuamini kuwepo Mungu ilikuwa sera rasmi ya serikali, na mamilioni ya watu waliokuwa wakimwamini Mungu waliuawa, kufungwa gerezani au kuteswa katika Urusi ya zamani.
Gazeti hilo limeeleza wasiwasi uliotanda kati ya wanasiasa wa Russia juu ya ushawishi wa "waabudu shetani," ambao wanawaona kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa na umoja watu wa Russia.
Ripoti ya gazeti hilo imesema, Andrey Kartapolov, mbunge mashuhuri wa Russia, amehusisha ibada ya mashetani na "Umoja wa Magharibi," akisema kwamba ibada hiyo inafadhiliwa na mataifa ya Magharibi kama sehemu ya vita vya kiitikadi dhidi ya Russia.
Gazeti la Times limesema kuwa serikali ya Russia inachunguza sheria za kupambana na waabudu mashetani na itikadi nyingine potovu, likiashiria hatua zilizochukuliwa hapo awali dhidi ya vuguvugu la kimataifa la LGBT.

Baadhi ya wabunge pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu "mahafali za kingono za kishetani" na uwezekano wa shirika la ujasusi la Ukraine kupenya na kuingia katika jamii za waabudu mashetani za Russia.