China yapuuza vikwazo vya Marekani, yanunua mafuta ya Iran kwa wingi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i125050-china_yapuuza_vikwazo_vya_marekani_yanunua_mafuta_ya_iran_kwa_wingi
Licha ya vitisho vya vikwazo kutoka kwa Marekani, uagizaji wa mafuta ya Iran na China umeongezeka kwa kasi kubwa mwezi Machi. Kwa mujibu wa mashirika ya kufuatilia meli za mafuta, China imeongeza ununuzi wake wa mafuta kutoka Iran, wakati mvutano wa kibiashara kati yake na Marekani.
(last modified 2025-04-11T22:48:45+00:00 )
Apr 11, 2025 22:48 UTC
  • China yapuuza vikwazo vya Marekani, yanunua mafuta ya Iran kwa wingi

Licha ya vitisho vya vikwazo kutoka kwa Marekani, uagizaji wa mafuta ya Iran na China umeongezeka kwa kasi kubwa mwezi Machi. Kwa mujibu wa mashirika ya kufuatilia meli za mafuta, China imeongeza ununuzi wake wa mafuta kutoka Iran, wakati mvutano wa kibiashara kati yake na Marekani.

Takwimu kutoka kampuni ya Vortexa zinaonesha kuwa China iliagiza zaidi ya mapipa milioni 1.8 ya mafuta kutoka Iran kwa siku katika mwezi wa Machi pekee.

Kwa upande mwingine, kampuni ya uchambuzi ya Kpler inaweka kiwango hicho kuwa mapipa milioni 1.37 kwa siku, ongezeko la asilimia 83 kutoka mapipa 747,000 mwezi Februari , hiki kikiwa ni kiwango cha juu zaidi ndani ya miezi mitano.

Kwa mujibu wa Kpler, mafuta ya Iran yalichangia asilimia 13 ya mafuta yote ghafi yaliyoingizwa China mwezi Machi.

China inaendelea kupuuza vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran, na inaelezwa kuwa kwa wastani China huagiza mapipa milioni 40 ya mafuta kutoka Iran kila mwezi.

Tangu Februari, utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umeweka awamu nne za vikwazo dhidi ya biashara ya mafuta ya Iran, ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya "shinikizo la juu kabisa" dhidi ya Tehran. Vikwazo vya karibuni vililenga kiwanda cha kusafisha mafuta cha Shouguang Luqing Petrochemical kilichopo mkoa wa Shandong, China.

Alhamisi, Marekani ilipanua orodha ya waliolengwa kwa vikwazo kwa kujumuisha mitandao ya biashara ya mafuta ya Iran — ikiwemo kituo cha kuhifadhi mafuta ghafi nchini China, ambacho kimeunganishwa moja kwa moja na bomba la mafuta linalopeleka kwenye kiwanda huru cha kusafisha mafuta.

Aidha, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimweka katika orodha ya vikwazo mfanyabiashara raia wa India, Jugwinder Singh Brar, anayeishi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa madai ya kuhusika na usafirishaji wa mafuta ya Iran kupitia meli zake karibu 30.

Hatua hii ya Marekani imekuja huku sera za Rais Trump za kuongeza ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini humo zikiendelea kuyumbisha biashara ya dunia. Katika wiki iliyopita, sera hizi zimeibua dhoruba kubwa katika anga za biashara ya kimataifa. Trump amelegeza msimamo na kusema amesitisha sera hiyo kwa muda wa siku 90 ingawa amepandisha ushuru wa bidhaa za China kwa asilimia 145

China nayo haikukaa kimya. Ijumaa, imetangaza kupandisha ushuru kwa bidhaa kutoka Marekani hadi asilimia 125 — hatua ambayo imezidisha mvutano katika vita vya kibiashara kati ya mataifa haya mawili.

Tume ya Ushuru ya Baraza la Serikali la China imesema kuwa uamuzi wa Marekani kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa kutoka China unakiuka sheria za biashara ya kimataifa, kanuni za uchumi na hata mantiki ya kawaida. Ushuru huo mpya uliowekwa na China dhidi ya Marekani unatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi Jumamosi hii.