Wananchi wa Pakistan na UK waandamana kulaani jinai za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i125066-wananchi_wa_pakistan_na_uk_waandamana_kulaani_jinai_za_israel
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Pakistan waliandamana jana baada ya Sala ya Ijumaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na mauaji ya umati yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Ghaza.
(last modified 2025-04-12T03:13:09+00:00 )
Apr 12, 2025 03:13 UTC
  • Wananchi wa Pakistan na UK waandamana kulaani jinai za Israel

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Pakistan waliandamana jana baada ya Sala ya Ijumaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na mauaji ya umati yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Ghaza.

Sambamba na Islamabad, mji mkuu wa Pakistan, miji ya Karachi, Lahore na Peshawar pia imeshuhudia maandamano ya watu wenye hasira waliotangaza mshikamano madhubuti na wananchi madhulumu wa Palestina.

Waandamanaji hao wamesikika wakitoa maneno ya kuilaani Israel na waungaji mkono wake na kubeba mabango ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani vikali kimya na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na Magharibi kwa jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni. Huko Islamabad, waandamanaji walikusudia kuelekea kwenye Ubalozi wa Marekani, ​​lakini walizuiwa na polisi.

Maandamano makubwa ya wananchi wa Uingereza ya kuiunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel

 

Katika upande mwingine, makundi mbalimbali ya wananchi wa Uingereza yamefanya maandamano makubwa katika barabara za London, mji mkuu na miji mingine ya Uingereza kulaani mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Makundi tofauti ya wananchi wa Uingereza kwa mara nyingine tena yamefanya maandamano makubwa mno huko London na katika miji mingine ya nchi hiyo ili kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina hasa wa Ghaza. Waandamanaji wameweka mashinikizo makubwa kwa serikali na wawakilishi wa majimbo ya Uingereza kuyataka yaache kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni.

Wananchi wa Uingereza wamesema: "Serikali yetu inaendelea kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kuupa silaha; uungaji mkono huu lazima ukome."