Amnesty: Jamii ya Kimataifa imefeli kuutatua mgogoro wa wakimbizi
(last modified Thu, 04 Aug 2016 15:05:51 GMT )
Aug 04, 2016 15:05 UTC
  • Amnesty: Jamii ya Kimataifa imefeli kuutatua mgogoro wa wakimbizi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limewakosoa viongozi wa dunia kwa kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa wakimbizi duniani.

Charlotte Phillips, mshauri wa masuala ya haki za wakimbizi wa shirika hilo nchini Uingereza amesema dunia inashuhudia mgogoro mkubwa wa wakimbizi ambao haujawahi kushuhudiwa katika muda wa miaka 70 iliyopita. Phillips ameyasema hayo baada ya mazungumzo ya maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kadhia ya wakimbizi na wahajiri kukosa kuzaa matunda.

Wahajiri wa Kiafrika wakielekea bara Ulaya

Katika kikao hicho cha Jumatano, wakuu wa nchi wanachama wa UN walishindwa kuafikiana namna ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo na kusema kuwa mkutano mwingine juu ya kadhia hiyo utafanyika mwaka 2018.

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni alibainisha kuwa, zaidi ya watu milioni 60 ulimwenguni ambao nusu yao ni watoto ni wahajiri au wakimbizi kutokana na kukimbia mateso na migogoro katika nchi zao.

Wanaokimbia mapigano Syria

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, hadi kufikia katikati ya mwezi Juni mwaka huu, karibu wahamiaji haramu elfu 50 kutoka nchi za Kiafrika waliwasili kwa boti barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean na kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka ujao 2016, bara hilo litakuwa limepokea zaidi wa wahajiri milioni moja na laki nne.

Tags