India na Pakistan zashutumiana kuvunja makubaliano ya usitishaji vita
Licha ya madai ya kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita kati ya Pakistan na India, lakini kila upande umekuwa ukiushutumu upande wa pili kuwa hauheshimu makubaliano hayo saa chache tu baada ya kufikiwa kwake.
Mataifa hayo mawili yenye nguvu za nyuklia yalifikia makubaliano ya kusitisha mapigano jana Jumamosi baada ya zaidi ya watu 60 kuuawa nchini India na Pakistan katika kipindi cha siku nne za mapigano ya mpakani.
Mapigano hayo yalikuja baada ya New Delhi kuanzisha mashambulizi kwa kile ilichodai kuwa watu wenye silaha wa upande wa Kashmir unaosimamiwa na Pakistan wameua watalii wa India na Nepal tarehe 22 mwezi uliopita wa Aprili, madai ambayo yamekanushwa vikali na Pakistan ambayo muda wote imekuwa ikiitaka serikali ya waziri mkuu wa India, Narendra Modi itoe uthibitisho wa madai yake hayo.
Baada ya kutangazwa kuanza kusimamishwa vita, kuliripotiwa ukiukwaji wa makubaliano hayo, hiyo hiyo jana Jumamosi huku miripuko ya silaha ikiendelea kusikika katika maeneo ya Kashmir inayodhibitiwa na India.
Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Vikram Misri amewaambia waandishi wa habari kwamba Pakistan imekanya maelewano yaliyofikiwa na nchi hizo mbili na kwamba wanajeshi wa India wamepewa amri ya "kukabiliana vikali" na mashambulizi ya Pakistan.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetoa taarifa mapema leo Jumapili kujibu madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa India na kusema kuwa, Islamabad imejitolea kuheshimu kikamilifu vipengee vya mapatano hayo na imeshutumu India kwa kutoheshimu makubaliano hayo katika baadhi ya maeneo.