UN: Ni "Uhalifu wa Vita" kuzuia chakula kuwafikia Wapalestina wa Gaza
(last modified Sat, 31 May 2025 07:59:34 GMT )
May 31, 2025 07:59 UTC
  • UN: Ni

Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya chakula kwa raia wa Palestina walioko kwenye njaa katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa ni uhalifu wa vita, hasa ikiwa inalenga kuwaondoa kwa lazima.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher, katika mahojiano aliyofanya Ijumaa amesema kuwa: “Tunaona chakula kikiwa kimekwama mipakani na hakiruhusiwi kuingia, wakati kuna watu upande wa pili wa mpaka wanaokufa kwa njaa. Wakati huohuo, tunawasikia baadhi ya mawaziri wa Israel wakisema kuwa hiyo ni njia ya kuwashinikiza Wapalestina wa Gaza."

Amesema: “Matumizi ya chakula kama silaha yanachukuliwa kama uhalifu wa kivita,” na kuongeza kuwa ni jukumu la mahakama na historia kutoa hukumu ya mwisho.

Katika siku za hivi karibuni, watu kadhaa waliokuwa wakijaribu kupata misaada ya kibinadamu wameuawa na vikosi vya Israel karibu na eneo la usambazaji wa msaada magharibi mwa Rafah, kusini mwa Gaza,  eneo ambalo sasa linadhibitiwa chini ya mpango wa pamoja kati ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

Mashirika ya misaada ya kimataifa tayari yameonya kuwa mipango ya Israel ya kudhibiti usambazaji wa misaada Gaza, ikiwemo ile inayoungwa mkono na Marekani, itazidisha mateso kwa watu wa Palestina walioko kwenye hali mbaya sana.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, amekosoa vikali mfumo mpya wa misaada unaoungwa mkono na Marekani, akisema kuwa ni "njia ya kupoteza mwelekeo na kufunika maovu yanayoendelea Gaza."

Israel ilizuia kabisa misaada kuingia Gaza tarehe 2 Machi, kabla ya kuanza tena mashambulizi ya kijeshi tarehe 18 Machi baada ya mazungumzo ya kusitisha mapigano kwa wiki sita kuvunjika.

Fletcher pia ameonya dhidi ya mpango wa Israel wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza.

Muungano wa kisiasa wa mrengo wa kulia unaoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu umeonyesha kuunga mkono mapendekezo ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kuwaondoa Wapalestina kabisa kutoka Gaza na kuigeuza kuwa eneo la kitalii kando ya bahari.