China: Marekani ndio chimbuko la ukosefu wa usalama Asia
(last modified Mon, 02 Jun 2025 02:17:43 GMT )
Jun 02, 2025 02:17 UTC
  • China: Marekani ndio chimbuko la ukosefu wa usalama Asia

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imelaani matamshi ya uingiliaji mambo ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani kuhusu Bahari ya Kusini ya China na kusisitiza kuwa: "Marekani ikiwa nchi  ya kibeberu imekuwa na mchango mkubwa katika kuyumbisha usalama wa Asia.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imetoa taarifa ikikosoa vikali matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani na kueleza kuwa, Washington inajaribu kuchafua na kupaka matope sura ya Beijing kwa tuhuma zisizo na msingi.

Taarifa hiyo ilisema kwamba Marekani sio tu kwamba, haijapuuza wito wa amani ya kikanda, lakini pia inaendelea kueneza fikra za vita baridi.

China imesisitiza kuwa, matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani yana uchochezi wa makusudi na yametolewa kwa lengo la kuleta hali ya wasiwasi na mifarakano katika eneo hilo.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, Washington imechochea kuongezeka kwa mvutano kwa kupeleka silaha za mashambulizi katika Bahari ya Kusini ya China.

Katika taarifa hiyo, China kwa mara nyingine tena imesisitiza kuwa, suala la Taiwan ni suala la ndani kabisa na kuionya Marekani kutoitumia Taiwan kama chombo cha mashinikizo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alidai siku ya Ijumaa katika mkutano na viongozi wa kijeshi wa Kusini-mashariki mwa Asia huko Singapore kwamba, Beijing imevuruga eneo hilo kwa "kunyanyasa majirani zake" katika Bahari ya Kusini ya China na kupanua haraka jeshi lake. Alionya kuwa, hivi karibuni jeshi la China linaweza kuidhibiti kwa nguvu Taiwan.