Uruguay yalaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel
Makundi mengi ya kisiasa na mirengo yameiitaka serikali ya Rais wa Uruguay Yamandu Orsi kuchukua msimamo mkali na mgumu zaidi dhidi ya uvamizi wa Israel huko Gaza.
Makundi yaliyotajwa yanajumuisha Chama cha Kikomunisti (PCU), Harakati ya Artigesta (VA), Chama cha Kisoshalisti (PS) na PVP, yameisisitiza kwamba kusonga mbele kwa Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi ni ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki.
Baada ya kikao, Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Uruguay ilitoa taarifa ikielezea hali ya Palestina kuwa ya kusikitisha sana na kutangaza kuwa Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina kupitia uvamizi wa kijeshi, na kuua zaidi ya watu 54,000 na kuwaweka wengine 71,000 katika hatari ya kufa kutokana na njaa.
Seneta wa Chama cha Kisoshalisti Gustavo Gonzalez pia alisema katika mahojiano na gazeti la La Diaria baada ya mkutano wa ndani wa chama hicho kwamba, anatumai baraza la mawaziri la Israel litalaaniwa na kukataliwa. Alibainisha: "Tunaamini kwamba ni lazima kuunganisha jamii na nguvu zote za mrengo wa kushoto katika kukabiliana na ukatili huu na hatuwezi kubaki bila ya kuwa upande wowote, kwa sababu tunakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu."
Gonzalez alisisitiza kuwa mauaji ya watoto, ulipuaji wa hospitali na shule ni jambo lisilohalalishwa hata kidogo hivyo ni lazima tusimame pamoja kwa ajili ya kuhakikisha vita na mauaji ya Israel katika Ukanda wa Gaza vinakomeshwa.