Mme na mke washushwa kwenye ndege Marekani, kisa Waislamu
Mwanamme mmoja na mkewe wa Marekani wameshushwa kwenye ndege ya shirika la Delta Airlines baada ya wahudumu kadhaa wa ndege hiyo kuwa na wasi wasi nao kwa kuwa ni Waislamu.
Wahudumu hao walimtaka rubani wa ndege hiyo awaagize Faisal Ali ambaye alikuwa anatumia simu yake ya rununu sambamba na kutamka neno 'Allah" mara kwa mara pamoja na mkewe Nazia Ali, aliyekuwa amevalia hijabu, wateremke kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikielekea mjini Cincinnati jimboni Ohio, ikitokea Paris Ufaransa Julai 26.
Raia hao wenye asili ya Pakistan licha ya kupewa uraia wa Marekani miaka 16 iliyopita, lakini walishangazwa na kitendo hicho cha kuagizwa kushuka kwenye ndege hiyo kwa kuonekana kuwa hatari kwa usalama kutokana na muonekano wao wa dhahiri na dini yao.
Hii ni katika hali ambayo, mwanamke mwingine Muislamu nchini Marekani ametimuliwa kazi na bosi wake baada ya kukataa kutii amri ya mkuu wake wa kazi iliyomtaka asijisitiri na kuvaa Hijabu akiwa kazini.
Bi Najaf Khan alikutana na mkasa huo zikiwa zimepita siku tatu tangu apate ajira katika kituo kimoja cha tiba ya meno mjini Viriginia huko Marekani. Bi Najaf Khan anasema kuwa, mkuu wake wa kazi alimwambia kwamba, huenda uvaaji wake wa Hijabu kazini ukawa ni bughudha na maudhi kwa wagonjwa wanokuja katika kituo hicho kwa matibabu ya meno hivyo ni bora asivae Hijabu akiwa katika mazingira ya kazini.
Julai 24, mamia ya Waislamu nchini Marekani waliandamana kupinga hatua za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika mji wa Washington DC huku wakipiga nara kulaani uenezaji wa vitendo vya chuki dhidi yao.
Ripoti ya mwezi Juni mwaka huu ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Berkeley jimboni California ilifichua kuwa, mashirika yapatayo 74 yametoa kiasi cha dola milioni 206 za Marekani kwa ajili ya kutumika kueneza chuki na hofu dhidi ya Uislamu nchini humo.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa, licha ya propaganda na uenezaji wa chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu, lakini dini hiyo ndiyo inayokuwa kwa kasi zaidi katika ulimwengu wa Magharibi.