UN yakemea vikali vikwazo vya Marekani dhidi ya majaji wa ICC
Volker Türk Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, amelaani uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Marekani wa kuweka vikwazo dhidi ya majaji wanne wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), akisema kuwa hatua hiyo inahatarisha misingi ya utawala bora na usimamizi huru wa haki.
Kauli ya Türk imekuja kufuatia tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, siku ya Alhamisi, akitangaza vikwazo dhidi ya majaji wa ICC wanaosimamia kesi zinazohusiana na uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, pamoja na hati za kukamatwa zilizotolewa na ICC dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, na aliyekuwa waziri wake wa vita, Yoav Gallant.
Türk amesema: “Ninasikitishwa sana na uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuwawekea vikwazo majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, hususan majaji wanawake wanne kutoka Benin, Peru, Slovenia, na Uganda, waliokuwa sehemu ya maamuzi kuhusu hali ya Afghanistan au Palestina."
Taarifa hiyo imesema vikwazo hivyo ni “jaribio la wazi la kudhoofisha uhuru wa chombo cha kimataifa cha utoaji haki, ambacho kinafanya kazi kwa mujibu wa mamlaka iliyotolewa na nchi wanachama 125 kutoka kila pembe ya dunia.”
Tangu Donald Trump arudi madarakani mwezi Januari, Marekani imeweka vizuizi mara kadhaa dhidi ya maafisa wa ICC. Ametoa amri kuu ya kiutendaji inayotishia kumuwekea vikwazo mtu yeyote anayeshirikiana na uchunguzi wa ICC, jambo ambalo limepelekea hata mashahidi kuogopa kujitokeza.
Baraza linalosimamia ICC, ambalo linawakilisha mataifa wanachama 125, pia lilitoa tamko siku ya Ijumaa likilaani vikali hatua ya Marekani ya kulipiza kisasi dhidi ya majaji wa mahakama hiyo.