WHO: Virusi vya Mpox bado ni tishio la afya kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127406-who_virusi_vya_mpox_bado_ni_tishio_la_afya_kimataifa
Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza kuwa, virusi vya Mpox bado ni tishio la afya kimataifa huku zaidi ya watu 37,000 wakiwa wameathirika na virusi hivyo.
(last modified 2025-06-10T08:32:38+00:00 )
Jun 10, 2025 08:32 UTC
  • WHO: Virusi vya Mpox bado ni tishio la afya kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza kuwa, virusi vya Mpox bado ni tishio la afya kimataifa huku zaidi ya watu 37,000 wakiwa wameathirika na virusi hivyo.

Mkurugezi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ametangaza kuongeza muda wa hali ya dharura wa kukabiliana na ugonjwa huo, baada ya mkutano na watalaamu wa kimataifa, ambao wamesema bado kuna ongezeko la maambukizo eneo la Afrika Magharibi na nje ya Afrika.

Shirika la Afya Duniani  (WHO) limesema tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza mwaka uliopita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ugonjwa huo umesambaa kwa mataifa zaidi ya 25, zaidi ya vifo 125 vikiripotiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kwa maambukizo na vifo, ikifuatiwa kwa karibu na Uganda, Burundi na kisha Sierra Leone.

Shirika hilo la afya duniani sasa linasema linafuatilia mwenendo wa maambukizo, hasa eneo la Afrika ya Magharibi na nje ya bara hilo, wakati huu baadhi ya mataifa yakiripotiwa kushindwa kufuatilia mwenendo wa maambukizo kutokana na ukosefu wa ufadhili.

Ugonjwa huo wa Mpox umeuwa watu 1,100 katika bara la Afrika tangu Januari mwaka jana.

Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao hapo awali ulijulikana kwa jina la ugonjwa wa tumbili, kabla ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kubadili jina lake mwaka wa 2022 kutokana na malalamiko kwamba jina hilo linaibua hisia za ubaguzi na unyanyapaa.

Ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kwa wanadamu kwa kuwasiliana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa au na mnyama mdogo wa mwituni, au kupitia vifaa vyenye maambukizi.